Baada ya kufanikiwa kuibuka na ushindi hapo jana katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya Ruvu Shooting, kocha mkuu wa klabu ya Yanga, Mwinyi Zahera amefichua siri nyingine juu ya nyota wake klabuni hapo.
Akizungumza kufuatia matokeo ya mchezo huo ambao Yanga ilitokea nyuma na kushinda mabao 3-2 katika uwanja wa taifa, Zahera amesema kuwa wachezaji wake ni wavumilivu licha ya ukata ilionao klabu hiyo, akisisitiza kuwa mchezaji yoyote akigoma kufanya mazoezi sababu ya kudai stahiki zake basi hatokuwa na haja ya kuendelea naye.
"Mnamuona Makambo, tokea alivyokuja alikuwa anakaa kwenye hoteli aliyofikia, juzi ndiyo pesa yake imetoka. Tangu alipokuja hakulipwa, na kulikuwa na deni kule kwao mpaka watu walikamata vitu vyake lakini ulishawahi kuona anakosa mazoezi?," ameuliza Zahera.
"Hakukosa mazoezi ni kwasababu alijua kocha amesema ukikosa mazoezi sababu ya kudai stahiki zako basi huwezi tena kucheza, utabaki huko huko nyumbani kwako. Mimi nacheza nahusika na wachezaji ambao wanajua kuvumilia, " ameongeza.
Baada ya ushindi huo wa jana, Yanga imeendelea kujikita kileleni mwa ligi kwa jumla ya 44 baada ya kushuka dimbani michezo 16, huku nafasi ya pili ikisalia kwa Azam FC yenye alama 40 baada ya michezo hiyo 16. Wapinzani wao Simba wameendelea kusalia nafasi ya tatu kwa alama 27 huku akiwa na viporo vya mechi nne.
Chanzo:Eatv
Social Plugin