Jeshi la Polisi mkoani Kagera, linamshikilia Kamugisha Kadodi (32), kwa tuhuma za kumshambulia mkewe, Kemilembe Paulo (30) na kusababisha kifo chake, chanzo kikidaiwa ni wivu wa mapenzi.
Mwanamke huyo alipigwa na mumewe wakiwa katika baa walipokwenda kunywa pombe ambapo mtuhumiwa alianza kumtuhumu mkewe kuwa ana uhusiano wa kimapenzi na mwanamme mwingine.
Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Revocatus Malimi, alisema tukio hilo la mauaji lilitokea Desemba 25, mwaka huu saa 11 jioni katika Kijiji cha Kigorogoro kilichoko mpakani mwa Tanzania na Uganda Wilaya ya Kyerwa.
Kamanda Malimi alisema siku ya tukio wanandoa hao waliondoka pamoja kwenda kunywa pombe baa kama sehemu ya kusherehekea sikukuu ya krismasi na wakiwa kule, ghafla ulizuka ugomvi uliosababisha mwanamke huyo kupigwa hadi kupoteza maisha pale pale.
Alisema mtuhumiwa huyo wa mauaji amekuwa akimtuhumu mke wake kuwa na uhusiano wa mapenzi na mwanamme ambaye hajafahamika ambaye Jeshi la Polisi bado linamfuatilia.
‘Mtuhumiwa tumemkamata kwa mahojiano zaidi, baada ya uchunguzi tutamfikisha mahakamani ili akakabiliane na mashtaka yatakayofunguliwa dhidi yake,” alisema.
Katika tukio la pili, Kamanda huyo alisema Justus Clemence (42), mkazi wa kitongoji cha Itokozi wilayani Biharamulo, alipoteza maisha baada ya kupigwa na watu waliomtuhumu kuiba kondoo wa mwanakijiji mwenzao.
Kamanda alisema uchunguzi unaendelea ili kuwabaini na kuwakamata waliohusika na mauaji hayo.
Katika tukio lingine, Kamanda Malimi alisema mtoto mmoja wa kiume aliokolewa juzi usiku kutoka katika shimo la choo, alikotupwa na mama yake mzazi muda mfupi baada ya kujifungua.
Kamanda Malimi alisema tukio hilo lilitokea katika Kijiji cha Mramba Kata Kihanga wilayani Karagwe na kwamba mtuhumiwa, Alisia Philemon (17), ameshakamatwa na anaendelea kuhojiwa na polisi.
Kamanda alisema kwa mujibu wa utetezi wa mtuhumiwa huyo, alifikia uamuzi huo baada ya kupewa ujauzito na mtu ambaye alimtelekeza.
“Tumeanza kumfuatilia mtu huyo anayedaiwa kuhusika na kumpa ujauzito huyu msichana ili atakapokamatwa afikishwe katika vyombo vya sheria,” alisema.
Social Plugin