ASKARI POLISI ATUPWA JELA KWA KUMUUA AFISA MTENDAJI HASANGA MBEYA


Wa kwanza kulia ni Juma Nestory (28) 

** 
Mahakama kuu kanda ya Mbeya imemuhukumu kwenda jela miaka kumi Askari wa Jeshi la Polisi G.4079, PC Juma Nestory (28) baada ya kupatikana na hatia ya kuua bila kukusudia.


Imeelezwa kuwa Nestory ambaye alikuwa mtumishi wa Jeshi la Polisi mjini Tunduma alimuua bila kukusudia Ofisa Mtendaji wa mtaa wa Hasanga, kata ya Uyole jijini Mbeya Clementina Mwonga.

Akitoa hukumu baada ya kusikiliza hoja za upande wa Mshtakiwa na upande wa Jamhuri, Jaji wa mahakama kuu kanda ya Mbeya, Mary Levira alieleza kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo kinyume na kifungu namba 195 na 198 cha kanuni ya adhabu.

Pamoja na hukumu hiyo, Jaji Levira amesisitiza kuwa mshtakiwa huyo ambaye ni mwenyeji wa Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu ana haki ya kukata rufaa ikiwa hatakuwa ameridhika na hukumu hiyo.

Upande wa Jamhuri uliongozwa na wakili Baraka Mgaya ulidai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Januari mosi mwaka 2017 wakati mshtakiwa akiwa na Marehemu ambaye alikuwa na mauhusiano naye ya kimapenzi.

Awali mshtakiwa alipopewa nafasi ya kujieleza alisema alikuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi na Marehemu Clementina na kwamba siku ya tukio walipanga kutoka wote kwa kuwa ilikuwa ni sikukuu.

Wakati wakiwa hotelini kwenye mapumziko walikunywa pombe kupita kiasi na ilipofika majira ya saa tano usiku baada ya kuona mpenzi wake amelewa alimtaka warudi nyumbani.

Alieleza kuwa wakati wakiwa njiani alimtaka marehemu kujua lini atamlipa fedha zake kiasi cha shilingi laki tatu na nusu alizomkopesha lakini marehemu akaapa kutompatia kwa kuwa ni mpenzi wake hali iliyopelekea kukasirika na kuchukua hatua ya kumpiga kwa kutumia ngumi sehemu mbalimbali za mwili wake hali iliyopelekea apoteze fahamu kwa muda wa dakika thelathini.

Nestory alisema aliamua kwenda kumtelekeza katika uwanja wa ndege wa zamani na yeye akakimbilia Tunduma usiku huo na siku moja baadaye alipata taarifa kwamba kuna mtu ameokotwa akiwa amefariki hatua iliyopelekea akimbilie nyumbani kwao Bariadi Mkoani Simiyu.

Wakili wa mshtakiwa huyo Mary Mgaya aliiomba mahakama kumpunguzia adhabu mshtakiwa kwa kutenda kosa bila kukusudia ikilinganishwa na mazingira ya tukio, pia ana familia ya mke, watoto na wadogo zake na amekiri kosa hilo licha ya kukaa mahabusu tangu Februari 28, 2017 alipokamatwa Mkoani Simiyu.

Kwa upande wake Wakili wa Serikali Baraka Mgaya aliiomba mahakama kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwa mshtakiwa na jamii nzima kutokana na watu kuendelea kujichukulia sheria mkononi na pia mshtakiwa alikuwa mtumishi wa Jeshi la Polisi kabla ya kuachishwa kazi kwa kosa hilo hivyo hakuonyesha kujutia kosa hilo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post