Kabla ya kuundwa kwa Jimbo kuu la Mbeya, Jimbo Katoliki la Iringa lilikuwa ni sehemu ya Jimbo kuu la Songea likiwa na Parokia 38, zinazohudumiwa na Mapadre wa Jimbo 72, Mapadre watawa 38, watawa wa kiume ni 332 na watawa wa kike ni 667.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko ameunda Jimbo kuu Jipya ya Mbeya nchini Tanzania linaloundwa na Jimbo Katoliki la Mbeya, Jimbo Katoliki la Iringa na Jimbo Katoliki la Sumbawanga. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu ametemua Askofu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga kuwa Askofu mkuu wa kwanza wa Jimbo kuu la Mbeya nchini Tanzania.
Kabla ya uteuzi huu, Askofu Nyaisonga ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, alikuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Mpanda. Jimbo kuu la Mbeya kwa sasa linaundwa na Parokia 48 zinazohudumiwa na Mapadre wa Jimbo 73, Mapadre watawa 15; lina watawa wa kiume 15 na watawa wa kike ni 299 kadiri ya takwimu za Kanisa kwa Mwaka 2018.
Kabla ya kuundwa kwa Jimbo kuu la Mbeya, Jimbo Katoliki la Iringa lilikuwa ni sehemu ya Jimbo kuu la Songea likiwa na Parokia 38, zinazohudumiwa na Mapadre wa Jimbo 72, Mapadre watawa 38, watawa wa kiume ni 332 na watawa wa kike ni 667. Jimbo Katoliki la Sumbawanga lilikuwa chini ya Jimbo kuu la Tabora likiwa na Parokia 21 zinazohudumiwa na Mapadre wa jimbo 53, Mapadre watawa ni 7; watawa wa kiume ni71 na watawa wa kike ni 348.
Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu mteule Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, alizaliwa kunako tarehe 3 Novemba, 1966, Wilayani Bunda, Mkoani Mara. Baada ya masomo yake ya msingi na sekondari, huko Mbeya na Sumbawanga, kunako Mwaka 1989 alijiunga na Seminari kuu ya Kibosho, Moshi, kwa ajili ya masomo ya Falsafa na baadaye akaendelea na masomo ya Kitaalimungu huko Segerea, Jimbo kuu la Dar es Salaam na hatimaye, kuwekewa mikono kama Shemasi, kunako mwaka 1995 baada ya kumaliza mwaka wa kichungaji, alioufanya katika Parokia ya Itaka, Jimbo Katoliki la Mbeya.
Tarehe 11 Julai, 1996 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre, Jimbo Katoliki la Mbeya na Hayati Askofu Yakobo Dominic Sangu. Historia inaonesha kwamba, huyu ndiye aliyekuwa Padre wa mwisho kuwekewa mikono na Hayati Askofu Sangu. Baada ya Upadrisho alifanya utume katika sehemu mbalimbali za Jimbo Katoliki Mbeya, kama Paroko usu huko Itumba na Mwalimu wa Seminari Ndogo ya Mbalizi. Kuanzia mwaka 1998 hadi mwaka 2001 alijiendeleza kwa masomo ya juu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tanzania, ambako alijipatia shahada ya kwanza. Baada ya masomo yake, alirudi kuendelea na kazi yake kama Mkuu wa shule ya Sekondari ya Pandahill, kuanzia mwaka 2001 hadi mwaka 2006.
Kuanzia mwaka 2006 hadi mwaka 2009 alijiendeleza kwa masomo ya juu zaidi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alikojipatia Shahada ya uzamili katika masomo ya Sayansi Jamii. Kuanzia mwaka 2009 hadi mwaka 2011 alikuwa ni Mhadhiri Msaidizi katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino cha Tanzania, SAUT, kilichoko Jijini Mwanza. Akiwa SAUT. Kunako Mwezi Agosti, 2010, alitumwa nchini Ujerumani kwa masomo ya juu zaidi, kama sehemu ya maandalizi ya kuwa ni Jaalimu wa Elimu hasa katika somo la Jiografia. Kabla ya kuhitimu masomo yake huko Ujerumani, tarehe 9 Januari 2011 akapokea simu kutoka kwa Balozi wa Vatican nchini Tanzania, ikimtaarifu kwamba, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI amemteua kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Dodoma na hatimaye, kuwekwa wakfu kama Askofu, tarehe 19 Machi 2011. Tarehe 17 Februari 2014, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Mpanda na kusimikwa rasmi tarehe 4 Mei 2014.
Askofu mkuu mteule Gervas Nyaisonga wa Jimbo kuu la Mbeya katika mahojiano maalum na Vatican News anasimulia kwamba, wito wake kama Mkatoliki na baadaye kama Padre na sasa kama Askofu na Askofu mkuu ni mchango mkubwa alioupokea kutoka kwa wazazi wake na kwa namna ya pekee Mama yake Mzazi aliyekuwa na nafasi ya pekee katika malezi. Huyu alikuwa kwa hakika ni Mwalimu na katekista wa kwanza katika majiundo yake ya maisha ya kiroho. Hii inatokana na ukweli kwamba, Baba yake Mzazi hakuweza kuwa nyumbani wakati wote kutokana na dhamana na utumishi wake kwa umma. Tangu akiwa mtoto mdogo alitamani na akapenda kutumikia Altareni pamoja na kusoma masomo Kanisani wakati wa Liturujia ya Neno la Mungu. Alipofikia umri wa kujiunga na Seminari ndogo, yeye alikuwa ni kati ya vijana kumi waliochaguliwa kutoka Parokiani mwake, lakini kati yao wawili tu, ndio waliobahatika kufikia Daraja Takatifu la Upadre, yaani Yeye Askofu mkuu mteule na Padre Januari Mwilwa wa Jimbo Katoliki la Mbeya.
Akiwa Seminari ndogo wito na ari ya kujitoa kwa ajili ya kumtumikia Mungu na jirani viliendelea kukua na kukomaa taratibu, akijikita zaidi katika maisha ya: Sala, Masomo, Kazi na Michezo, kama sehemu ya vipaumbele wakati wa malezi Seminarini. Ni mahali alipokuza vipaji vyake kwa ajili yake mwenyewe na Kanisa kwa ujumla. Akaendelea kukua katika kimo na busara sanjari na kukomaa kwa wito wake, akitamani daima kuwa Padre. Alipohitimu masomo ya kidato cha sita, alishawishiwa na walimu wake kwenda Jeshi la Kujenga Taifa kwa mujibu wa sheria, ili baadaye, aweze kujiunga na Chuo Kikuu kwa masomo ya juu zaidi. Mkurugenzi wa miito hakucheza mbali na vijana wake, akamshauri kujiunga na Seminari kuu kwa ajili ya kuendelea na masomo ya kipadre, ushauri huu ukajikita katika moyo wake, akapiga moyo konde na kwenda Seminarini.
Kwa sasa anamwimbia Mungu utenzi wa shukrani kwa matendo makuu aliyomtendea katika hija ya maisha yake kwa kumteuwa kuwa Askofu mkuu wa kwanza wa Jimbo kuu la Mbeya, muda wa mwezi mmoja tu tangu alipofariki dunia Askofu Evaristo Marcus Chengula, hapo tarehe 21 Novemba 2018. Hili ndilo Kanisa Katoliki la Tanzania: maajabu yaliyofanyika hata baada ya kufariki dunia kwa Kardinali Laurian Rugambwa, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, tarehe 8 Desemba 1997; Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa Askofu mkuu mwandamizi Polycarp Pengo kuwa Kardinali na kumsimika rasmi tarehe 22 Februari 1998.
Chanzo - Vatican News