Sakata la tuhuma dhidi ya kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bernard Membe, kuonyesha mapema nia ya kutaka urais katika uchaguzi ujao, limeelezwa kuwa ni mpasuko ndani ya chama hicho.
Mchambuzi wa masuala ya siasa nchini, Profesa Mwesiga Baregu, anasema kwa sasa ndani ya CCM, kuna makundi mawili yanayopingana na yameanza kujionyesha wazi.
Anayataja makundi hayo kuwa ni lile la wanaCCM ambao wamedumu katika chama kwa miaka yote wakati wa shida na raha na pia wapo wanaCCM wa kuja na kwamba makundi hayo yanapingana.
Mwanazuoni huyo anasema wanaCCM, ambao wamedumu ndani ya chama bila kuhama wanaitwa ‘CCM masalio’ na kwamba wale wanaorejea wanaitwa ‘CCM wakuja.’
Anasema haitatokea siku moja makundi hayo yakakubaliana, hivyo ana uhakika makundi na hata mpasuko ndani ya CCM vitaendelea kuwepo, iwapo hakutakuwa na juhudi za ziada za kumaliza tatizo hilo.
“Hata wito wa Katibu Mkuu wa CCM Dk. Bashiru Ally kwenda kwa Membe unaonyesha kuna mpasuko, kwa sababu Dk. Ally ni CCM wa kuja wakati Membe ni CCM masalio,” anasema Prof. Baregu.
Anabainisha kuna haja kwa CCM kujitathmini haraka na kuchukua hatua, kwa vile kitendo cha kumuita Membe ni dalili kuwa hali si shwari na ndiyo maana ya kutuhumiana wenyewe kwa wenyewe.
“Sakata hili linatoa fursa chanya kwa kambi ya upinzani endapo halitatafutiwa ufumbuzi mapema, kwani inaonyesha dhahiri kuwa ndani ya CCM bado kuna makundi...huu ni mwanzo na mwisho wa CCM, mambo yanaweza kuwa magumu kwa CCM, kwa sababu wanaweza kupata mgombea, ila asiungwe mkono,” anasema.
Anabainisha kuwa ki-fursa inaonyesha ni uwanja wa kucheza wa upinzani kwa madai kwamba huo mwendo ndani ya CCM si mzuri, unaweza kusababisha hali kuwa mbaya zaidi kufikia mwaka 2020.
Hivi karibuni kumezuka mvutano wa maneno baina ya Katibu Mkuu wa CCM Dk. Ally kutokana na namna alivyotumia mikutano ya hadhara kumuita Membe ofisini kwake, jambo ambalo Membe alilihoji kupitia akaunti yake ya twitter.
Membe alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa katika Serikali ya Awamu ya Nne na pia ni miongoni mwa wanachama waliokuwa wakitafuta kuwania urais kupitia CCM mwaka 2015, ingawaje kura zake hazikutosha katika ngazi ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).
Dk. Ally alimtaka afike ofisini kwake kujibu tuhuma zinazomkabili ikiwamo ya kupanga njama za kumkwamisha Mwenyekiti wa CCM Taifa, ambaye pia ni Rais wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli.
Tangu kumalizika kwa mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, mwanasiasa huyo amekuwa kimya hadi hivi karibuni alivyotuhumiwa kuanza mipango ya kutaka urais mwaka 2020.
Membe ni miongoni mwa makada wakongwe na viongozi wa CCM waliotuhumiwa kuwa wanahujumu chama hicho, akitajwa kufanya vikao vya chinichini kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 2020.
“Hao wanaopingana wamewahi kuwa viongozi wakubwa ndani ya CCM, inashangaza kuona wakitofautiana katika kujadili kile kilichofanywa na katibu mkuu wa chama chao,” anasema.
“Unasikia kuna kauli kwamba CCM imevamiwa na wasaka tonge, hii inatolewa na wanaCCM masalio, ambao sidhani kama itakuja kutokea wakakubaliana na hao wenzao wanaoitwa wa kuja,” anasema.
“Wakati makundi hayo yakipingana, ni nafasi kwa vyama vya upinzani kujipanga vizuri ili kuhakikisha unajiweka katika mazingira mazuri ya kujiongezea wanachama zaidi, hasa wenye nia ya kweli ya kuleta mabadiliko,” anasema.
Chanzo - Nipashe