Rais wa Uganda Yoweri Museveni amekutana na mlimbwende wa nchi hiyo ambaye hivi majuzi ameshinda taji la mlimbwende bora wa Afrika.
Quiin Abenakyo alitawazwa kuwa Miss Uganda mwezi Agosti na kushiriki shindano kubwa la ulimbwende duniani la Miss World nchini Uchina mwezi huu ambapo aliingia kwenye tano bora na kutawazwa taji la Miss Africa.
Bi Abenayako amerejea Uganda jana, na saa chache baadae akaenda Ikulu kukutana na rais Museveni.
Rais Museveni alimsifia mlimbwende huyo na waandaji wa shindano la Miss Uganda na kuahidi kuwapa ushirikiano. Lakini hata hivyo 'alimsuta' mrembo huyo kwa kuvaa "nywele za Kihindi".
"Abenakyo ni mrefu haswaa, binti mrembo kutoka Musoga. Tatizo langu pekee ni kuwa alikuwa amevaa nywela za Kihindi. Nimemsihi kubaki na nywele zake za asili. Lazima tuuoneshe uzuri wa Kiafrika katika uhalisia wake," ameandika Museveni kupitia ukurasa wake rasmi wa Twitter.
Ujumbe huo wa Museveni umeibua mjadala nchini Uganda ambapo watu wengi wanamuunga mkono kutaka wasichana kuacha mawigi. Hata hivyo kuna kundi kubwa la watu ambao wamechukulia kauli hiyo ya Museveni kama kichekesho.
Museveni anajulikana kwa kuongea kile atakacho bila kujali maoni ya watu yatakavyokuwa dhidi yake.
Mkutano wa wawili hao ulifanyika katika Ikulu ya Entebbe. Museveni alimpongeza mrembo huyo kwa kumaliza masomo yake ya shahada hivi karibuni akisema kuwa mlimbwende huyo ni: "kielelezo cha msemo wa uzuri uliombatana na akili."
Chanzo- BBC
Chanzo- BBC
Social Plugin