Kiungo wa Real Madrid na timu ya taifa la Croatia Luka Modric ameshinda tuzo ya Ballon d'Or kwa mwaka 2018, na kuwa mchezaji wa kwanza tofauti na Lionel Messi na Cristiano Ronaldo kushinda tuzo hiyo baada ya miaka 10.
Modric, 33, ameshinda kombe la Klabu Bingwa Ulaya mwezi Mei kwa mara ya tatu mfululizo na kulisaidia taifa lake kufika hatua ya fainali katika michuano ya Kombe la Dunia.
Mchezaji wa zamani wa Brazil na AC Milan Kaka, alishinda tuzo hiyo mwaka 2007, na baada ya hapo Messi na Ronaldo wameshinda mara tano kila mmoja tuzo hiyo ya thamani kabisa kwa wachezaji wa kandanda duniani.
Ronaldo, ambaye amehamia Juventus msimu huu amemaliza katika nafasi ya pili mwaka huu, huku Messi akishika nafasi ya tano. Nafasi ya tatu ameshika mshambuliaji wa Atletico Madrid Antoine Griezmann huku mshambuliaji wa PSG Kylian Mbappe akishika nafasi ya nne - wawili hao walikuwa sehemu ya kikosi cha Ufaransa kilichoshinda Kombe la Dunia mwaka huu.
Huu umekuwa mwaka wa kutuzwa kwa Modric ambaye awali alishinda tuzo ya FIFA ya mchezaji bora wa kiume na pia alishinda tuzo ya mchezaji bora wa michuano ya Kombe la Dunia.
Chanzo:Bbc