Nyumba na gari vikiwa vimeungua
Watu zaidi ya 20, wakazi wa kijiji cha Nzera Kata ya Nzera, Wilayani Geita hawana sehemu ya kuishi kufuatia nyumba zao kubomolewa na zingine kuchomwa moto na kikundi cha watu ambao pia ni wakazi wa eneo hilo.
Tukio hilo limehusisha kubomolewa kwa nyumba zaidi ya nne na zingine kuchomwa moto kwa kile kinachoelezwa kuwa ni chuki binafsi zinazohusisha masuala ya kisiasa.
Mbali na nyumba hizo kubomolewa na zingine kuchomwa moto, pia magari mawili aina ya Hiace T 226 GBV na Noah, mali ya Mratibu Elimu Kata ya Katoma, Kulwa Sherembi yamechomwa moto.
Jeshi la Polisi limewakamata watu 25 wanaohusishwa na tukio hilo huku likilaani vikali kitendo hicho ilichokiita ni cha kishenzi na kuahidi kuwasaka watu wote waliohusika na kuwatia mbaroni.
Akifafanua kuhusiana na tukio hilo, lililotokea majira ya alfajiri, Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Mponjoli Mwalubambo amesema chanzo cha tukio hilo ni uvamizi uliotokea, ambapo vibaka walivamia nyumba mbili za wakazi wa eneo hilo, Faustine Kaswahili na Edward Samson kisha kujeruhi na kupora fedha na kutokomea kusikojulikana.
Baada ya tukio hilo ndipo kikundi kingine kilipojihamasisha na kwenda kubomoa na kuchoma nyumba hizo pamoja na magari kikiwahusisha wamiliki wa familia hizo kufadhili waharifu wa uvamizi uliotokea kijijini hapo ili hali wakijua si kweli.
Social Plugin