Klabu ya soka ya Mtibwa Sugar imetangaza nia yake ya kujenga uwanja wa kisasa na mkubwa wa soka, ambao utakuwa na uwezo wa kubeba mashabiki wengi zaidi.
Hayo yamezungumzwa na Mkurugenzi wa klabu hiyo, Jamal Bayser ambapo amesema kuwa wameamua kuwafuata mashabiki wao na wapenda soka kwa kuwajengea uwanja karibu na makazi yao.
"Dhumuni letu hasa ziadi ni kujenga uwanja ambao utakuwa karibu zaidi kule na wananchi, kule kuna maeneo wanaita Mabawa, ni eneo ambalo wananchi wengi wa Madizini pale wanaweza kutembea kidogo kuliko kule Manungu ambako ni ni mbali kwao," amesema Mkurugenzi huyo wa Mtibwa.
Mtibwa Sugar inajiandaa kwaajili ya mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya KCCA ya Uganda utakaopigwa wikiendi hii Jijini Dar es salaam.
Katika mchezo wa kwanza uliofayika mjini Kampala Uganda wikiendi iliyopita, Mtibwa Sugar ilifungwa kwa mabao 3-0, ambapo katika mchezo wa marudiano inahitaji ushindi wa mabao 4-0 ili iweze kusonga mbele katika hatua inayofuata.