Rais wa Urusi Vladimir Putin ameitaka serikali yake kuchukua hatua dhidi ya muziki wa kufoka foka.
Japo matamasha kadhaa ya muziki huo yamezuiwa katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo katika siku za hivi karibuni, jitihada za serikali kuupiga marufuku kabisa zimegonga mwamba.
Sababu marufuku ya serikali imeshindikana, Putin anataka mamlaka zifanye kazi ya ziada kuudhibiti.
"Wizara ya Utamaduni itatafuta namna bora ya kusimamia matamasha ya vijana," amesema Putin.
Kauli ya Putin inakuja siku chache baada mwanamuziki wa maarufu wa rap nchini humo anayefahamika kama Husky kukamatwa baada ya matamasha yake kufutwa.
Awali mwezi huu wa Disemba mamlaka katika jiji la kusini la Krasnodar zilizuia tamasha la Husky kwa kile walichokiita "msimamo mkali".
Mwanamuziki huyo ambaye jina lake halisi ni Dmitry Kuznetsov - alikonga nyoyo za mashabiki wake kwa kutumbuiza kutoka juu ya gari.
Chanzo:Bbc