Mvutano kati ya katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally na waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Serikali ya Awamu ya Nne, Bernard Membe umechukua sura mpya baada ya katibu mkuu mstaafu wa chama hicho, Yusuf Makamba kuunga mkono utaratibu uliotumiwa na mhadhiri huyo wa zamani wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Kauli ya Makamba imekuja ikiwa ni siku moja baada ya katibu mtendaji mwingine mstaafu wa CCM, Pius Msekwa kukosoa utaratibu uliotumiwa na Dk Bashiru akisema alipaswa kumpigia simu au kumwandikia barua ya wito.
Hivi karibuni akiwa mkoani Geita kwenye mkutano mkuu wa CCM wa mkoa, Dk Bashiru alimtaja Membe akisema anatajwa kumkwamisha Rais John Magufuli na amekuwa akiratibu mbio za kuusaka urais mwaka 2020, kisha akamtaka kufika ofisini kwake ili wazungumze.
Akizungumza kwa simu na Mwananchi jana, Makamba alisema Dk Bashiru ni mtendaji mkuu wa chama anayewakilisha Halmashauri Kuu na Mkutano Mkuu, hivyo ana mamlaka ya kumuita mwanachama yeyote hata ikiwa hadharani.
Makamba aliongeza kuwa hata yeye alipokuwa katibu mkuu alikuwa akiwaita wanachama hivyohivyo na kwamba, hata aliwahi kuitwa na viongozi wa Tanu.
“Mimi niliwahi kuitwa na (John) Mhavile, nilikuwa mkuu wa Wilaya ya Tanga. Mhavile alikuwa katibu mtendaji wa Tanu, yalitokea maneno pale Tanga nikaambiwa njoo, tena si kwa simu. Niliwahi kuitwa na Mwakawago (Balozi Daudi). Kwa hiyo haya mambo siyo kwamba ni ya jana,” alisema Makamba.
Akifafanua zaidi, alisema aliitwa na Mhavile mwaka 1974. “Mzee Mhavile akaja Mkwakwani (Tanga) akasema palepale kama kuna mkuu wa wilaya yupo hapa na asikie, aje Dodoma. Hakuna aliyelalamika kwamba kwa nini nimeitwa hadharani.”
Mbali na Mhavile, Makamba pia alisema mwaka 1978 akiwa mkuu wa Wilaya ya Kasulu aliitwa na Pius Msekwa aliyekuwa katibu mtendaji wa CCM.
“Niliwahi kuitwa na Msekwa kwamba njoo Dodoma na nikaenda. Kwa hiyo ni utaratibu haukuanza jana.”
Hata hivyo, Makamba alibadilisha kauli yake ya awali na kusema aliitwa na Msekwa katika ofisi za CCM zilizopo Lumumba, Dar es Salaam na alikwenda.
“Kwa hiyo kuitwa na wakubwa ni jambo la kawaida, msiwaonee kwa njia waliyotumia. Kubwa katibu mkuu yuko sahihi. Mimi niseme nini? Katibu mkuu amemwita Membe na aliyeitwa ameshakubali kwenda, utaratibu ndiyo huo,” alisisitiza huku akitoa mifano ya maandiko ya Biblia.
“Hivyo ndivyo maandiko yanavyosema, tuitii mamlaka iliyowekwa na hayo ndiyo mamlaka aliyonayo katibu mkuu. Hata mimi niliwahi kuwa katibu mkuu niliwaita watu.”
Akifafanua zaidi kupitia mifano ya Biblia, Makamba aliwalaumu watu wanaomkosoa Dk Bashiru akisema hawakosi la kusema.
“Alikuja Yohana Mbatizaji alikuwa akiishi msituni na alikuwa hali, bali anafunga, watu wakamwita kichaa. Akaja Bwana Yesu akawa anakula watu wakasema mlafi,” alisema Makamba.
Na Elias Msuya, Mwananchi