LAZARO NYALANDU ATAKA WATANZANIA KUMUOMBEA MBOWE,MATIKO

Waziri wa zamani Lazaro Nyalandu leo Jumapili Desemba 2, 2018 amewataka Watanzania kuwaombea watu waliowekwa kizuizini nchini Tanzania akiwemo mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, mbunge huyo wa zamani wa Singida Kaskazini ameandika, “Jumapili ya leo tuungane sote kumwombea mwenyekiti Mbowe, Matiko na wote waliowekwa kizuizini popote Tanzania.”

“Kwa sababu moja, au nyingine imeandikwa haki huinua Taifa. Wenye Mamlaka wakaone fahari kutenda haki bila kukawia zaidi. Kama Taifa, tusimame pamoja nao.”

Mbowe na Matiko walifutiwa dhamana na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, anayesikiliza kesi hiyo Novemba 23, 2018 kutokana na maombi ya upande wa mashtaka yaliyodai wameshindwa kuhudhuria mahakamani bila sababu za msingi katika kesi yao iliyopangwa kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali.

Viongozi hao wamekata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam chini ya hati ya dharura wakipinga uamuzi wa Mahakama ya Kisutu kuwafutia dhamana katika kesi ya jinai inayowakabili mahakamani hapo.

Juzi, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilisimamisha usikilizaji wa rufaa ya Mbowe na Matiko hadi rufaa ya Serikali itakapoamuliwa na Mahakama ya Rufani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم