Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, ametembelea mashamba darasa ya zao la pamba katika vijiji vya Masengwa na Ikonda vilivyopo kwenye Kata ya Masengwa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga kwa ajili ya kutoa elimu kwa vitendo kwa wakulima ili kulima kilimo cha kisasa ambacho kitawapatia mavuno mengi.
Mboneko amefanya ziara hiyo jana Desemba 7,2018 akiambatana na maofisa ugani wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, kata pamoja na mtaalamu kutoka bodi ya Pamba Thomas Tiluhongelwa, kwa kutembelea mashamba darasa ili kutoa elimu kwa wakulima kwa vitendo, na kulima kilimo chenye tija ambacho kitawainua kiuchumi.
Akizungumza mara baada ya kutembelea mashamba hayo darasa ya zao la pamba kwa kutoa elimu kwa vitendo kwa wakulima, kulima kisasa kwa kupanda mbegu kwa mstari kwa kutumia kamba, Mboneko alisema Serikali imedhamiria kuwa na wakulima bega kwa bega, kwa kuhakikisha kilimo chao kina kuwa na faida na kuwatoa kwenye umaskini.
Alisema kilimo ndiyo uti wa mgongo kiuchumi kwa taifa, na ndiyo maana wameamua kutoka maofisini na kwenda mashambani kutoa elimu kwa vitendo kwa wakulima ili kulima kisasa na kuachana na kilimo cha mazoea, ambacho kimekuwa kikiwapatia mavuno kidogo na kuendelea kuwa na maisha duni.
“Tumekuja kuwaonyesha wakulima namna ya kupanda mbegu kisasa kwa kutumia kamba, ili kilimo chao kiwe na tija kwa kupata mavuno mengi na kuwainua kiuchumi,”alisema Mboneko.
“Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli, imedhamiria kuwainua wakulima kiuchumi kwa kuwatatulia changamoto ambazo zimekuwa zikiwakabili, hivyo na sisi kama viongozi ambao tunamsaidia Rais tunapaswa kutoka maofisini na kwenda mashambani kutoa elimu kwa vitendo namna ya kulima kisasa,”aliongeza.
Pia alitoa wito kwa wakulima pale wanapomaliza kuvuna mazao yao wasafishe mashamba yao mapema kwa kuchoma moto masalia ili kuondoa tatizo la wadudu ambao wamekuwa wakishambulia mbegu na kusababisha kushidwa kuota vizuri.
Naye mmoja wa wakulima Edward Ngeleja ambaye alihudhuria mafunzo hayo ya kilimo cha kisasa kwa vitendo, alisema yatamsaidia kuinuka kiuchumi kwa kupata mavuno mengi ambapo hekari moja unaweza kupata kilo 700 hadi Tani moja, tofauti na kilimo cha mazoea ambacho hekari moja hupata kilo 250.
Kwa upande wake Ofisa kilimo wa Kata hiyo ya Masengwa Amedius Lumanyika, alisema kilimo hicho cha kisasa kimekuwa kikisaidia wakulima kupata mavuno mengi na kuinua uchumi wao na kata kwa ujumla ,ambapo mwaka jana walivuna tani 600 na mwaka huu wameongeza Tani 800.
TAZAMA PICHA ZA MATUKIO HAPA CHINI
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko(kushoto) akiwa na afisa Kilimo Kata ya Masengwa Diokresi Kawamala wakipima kamba kwa futi, na kuanza kutoa elimu kwa wakulima kwa vitendo namna ya kupanda mbegu kwa kufuata kilimo cha kisasa ambacho kitakuwa na tija kwao kwa kupata mavuno mengi na kuinuka kiuchumi.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akichimba mashimo kitaalamu kwa ajili ya kupanda mbegu ya zao la pamba katika shamba la mfano ili kutoa elimu kwa wakulima kwa vitendo kulima kisasa.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akipanda mbegu za pamba kitalaamu ili kuonyesha mfano wakulima namna ya kupanda mbengu hizo ambazo zitawapatia mavuno mengi.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akionyesha nyenzo ya kutengeneza Kamba kwa ajili ya kuifunga mashambani kwa kuonyesha vipimo sahihi kwa ajili ya kupanda mbegu za pamba kitaalamu.
Wakulima wakipanda mbegu za pamba kwa njia ya kitaalamu mara baada ya kumaliza kupewa elimu hiyo kwa vitendo na mkuu huyo wa wilaya.
Wananchi wakiendelea kupanda mbegu za pamba kwa njia ya kitaalamu.
Wakulima wakiwa kwenye eneo la shamba la mfano kwa ajili ya kupewa elimu ya kilimo cha kisasa na chenye tija, ili kuondokana na kilimo cha mazoea ambacho kimekuwa kikiwafanya kuendelea kuwa maskini kwa kulima mashamba makubwa na kupata mavuno kidogo.
Mkulima wa zao la pamba katika kijiji cha Masengwa Edward Ngeleja akielezea namna alivyoanza kupata faida kwa kulima kitaalamu tofauti na zamani alivyokuwa akilima kwa mazoea, kuwa awali hekari moja alikuwa akipata Kilo 250 hadi 300, lakini mara baada ya kuanza kulima kitaalamu hekari moja amekuwa akipata kilo 700 hadi tani moja.
Hassani Kasomi ni mmoja wa wakulima ambao wamekwenda kupata elimu namna ya kulima kisasa kwa kupanda mbegu za pamba, na kuipongeza Serikali kwa kuwajali wakulima kuwainua kiuchumi.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akiwa kwenye Shamba la mkulima Edward Keni, ambalo lilipandwa kimazoea na kuwa chafu, na hivyo kusababisha panya kula mbegu zote za Pamba zilizopandwa katika hekari zake saba.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akiwa na afisa tawala wilaya hiyo Charles Maugira wakitoa elimu kwa vitendo namna ya kusafisha shamba kwa kuzoa masalia yote ya mavuno, ili kuondoa changamoto ya kuwapo kwa Panya kwenye mashamba na kutoshambulia mbegu tena.
Zozezi la usafishaji shamba ukiendelea, na kutolewa wito kwa wakulima pindi wanapomaliza mavuno mashambani wazoe masalia na kuyachoma moto.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akiongoza zoezi la uchomaji moto masalia ya mavuno shambani.
Mkulima wa zao la pamba Edward Keni akielezea namna panya walivyokula mbegu zake za pamba mara baada ya kuzipanda bila ya kulisafisha shamba lake lenye hekali Saba.
Afisa kilimo wa Kata ya Masengwa Amedius Lumanyika akielezea namna wanavyotoa elimu kwa wakulima katika Kata hiyo kufuata kilimo cha kisasa.
Kaimu afisa kilimo wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Ibrahimu Bundo, akielezea namna Serikali inavyojitahidi kuhamasisha wananchi waendelee kulilima zao hilo la pamba, ambalo ndio litawainua kiuchumi, na kubainisha msimu wa mwaka jana kulikuwa na wakulima wa pamba 1,650, lakini mwaka huu wameongezeka na kufikia 2,118 .
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akizungumza na wananchi wa Masengwa kwenye mkutano wa hadhara, na kuwataka wafuate maelekezo ya wataalamu kulima kisasa, kilimo ambacho kitakuwa na tija kwao kuwainua kiuchumi kutokana na kupata mavuno mengi.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko akinunua maembe yote kwenye kichanja mara baada ya kumaliza mkutano huo wa hadhara ,na kisha kuwagawia wananchi wa Kijiji na Kata hiyo ya Masengwa.
Na Marco Maduhu-Malunde 1 Blog.
Social Plugin