Jeshi la Polisi Jijini Dodoma, limepiga marufuku kwa wananchi kula nyama ya mbuzi ambao walikufa kwenye ajali, iliyohusisha malori mawili hapo jana.
Marufuku hiyo imetolewa na Kamanda wa Polisi Dodoma, Gilles Murotto, na kusema kwamba daktari amewaambia kuwa nyama hiyo imeingia sumu baada ya kumwagikiwa mafuta ya dizeli, yaliyomwagika kwenye moja ya malori yaliyopata ajali.
“Hiyo ajali ilihusisha malori mawili ambayo moja lilikuwa limebeba mbuzi 150 likielekea Dar es salaam, na lingine likiwa ni la tanki la mafuta, yalivyogongana mbuzi 11 wamekufa na baadhi ya watu walijeruhiwa pia, hivyo tumetahadharisha watu kula nyama yake, kwanza ni ina dizeli na pia hata daktari kasema ina sumu ni hatari kwao”, amesema Kamanda Murotto.
Akielezea ajali hiyo Kamanda Muroto amesema imetokea jana majira ya saa 4 usiku jijini Dodoma, na majeruhi wote ambao walikuwa watano walikimbizwa kwenye hospitali ya Rufaa ya Dodoma, na hali zao zinaendelea vizuri.