Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko amewaonya baadhi ya askari wa Kituo cha Polisi Kata ya Salawe kutumiwa na viongozi kwenda kuvuruga amani kwa wananchi, kinyume cha maadili ya kazi yao inayowataka kulinda usalama wa raia na mali zao.
Inadaiwa diwani wa kata hiyo, Joseph Buyugu anawatumia baadhi ya askari kuonea wananchi hasa wanaofichua maovu kwenye mikutano ya hadhara ya viongozi wakuu kwa kuwapiga na kisha kuwatia mbaroni.
DC Mboneko ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama alitoa onyo hilo juzi wakati alipofanya mkutano wa hadhara wa kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua kwenye kata hiyo, ambapo hivi karibuni kulitaka kutokea machafuko ya amani kwenye eneo hilo.
Alisema amesikitishwa na viongozi wa maeneo hayo kulitumia Jeshi la Polisi vibaya kutaka kuvuruga amani ya nchi na kujichukulia mamlaka ambayo yapo nje ya utawala wao kwa kuwapiga wale ambao wamekuwa wakifichukua maovu yao pamoja na kuwavunjia nyumba wananchi na kuharibu mali zao.
“Jeshi la Polisi nawaonya msitumiwe na viongozi kuvuruga amani ya nchi ninyi kazi yenu ni kudumisha amani na kulinda usalama wa raia na mali zao na si vinginevyo, acheni kutumika kuonea wananchi pamoja na kuwaomba rushwa, kama mnaona mishahara yenu haitoshi acheni kazi,” alisema Mboneko.
“Na nyie viongozi msiwe chanzo cha machafuko ya kuvuruga amani kwa wananchi, kazi yenu ni kuwatumikia na kutatua kero zao pamoja na kuwa hamasisha kwenye masuala ya maendeleo, na siyo kugeuka miungu watu na kuanza kuwaonea huku mkiwapiga, kuwavunjia nyumba zao, na kisha kuwasweka rumande,” aliongeza.
Awali baadhi ya wananchi wa kata hiyo ya Salawe wakiwakilisha kero zao kwa mkuu huyo wa wilaya akiwamo Seke Nyeke na Dumila Hamis, alisema malalamiko yao mengi yalikuwa ni viongozi wa maeneo hayo akiwamo na diwani wamekuwa wakishirikiana na askari Polisi kuwaonea na ili kutoka rumande, lazima watoe kitu kidogo.
Kwa upande wake, diwani Buyugu alikana tuhuma hizo za kulitumia Jeshi la Polisi kuvuruga amani huku Kamanda wa Polisi Wilaya ya Shinyanga, Claud Kanyolota akiwaonya askari hao kutorudia tabia hiyo na kubainisha malalamiko hayo atayafanyia kazi ili wachukuliwe hatua za kinidhamu.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Ngassa Mboje alisikitishwa na kitendo cha diwani wa Salawe aliyechaguliwa na wananchi na matokeo yake kuwakandamiza huku tatizo hilo limeonekana analifanya kwa wale ambao ana chuki nao, jambo ambalo halifai na ni hatari alimuomba aache tabia hiyo ili wananchi waishi kwa amani.
Social Plugin