Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli ameliagiza Jeshi la Polisi kuimarisha nidhamu kwenye uchaguzi ujao wa serikali za Mitaa wa mwaka 2019.
Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo Desemba 21, 2018 katika mahafali ya kuhitimisha mafunzo ya Maofisa na Wakaguzi Wasaidizi wa Polisi, ambapo amesema kuna baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakilituhumu jeshi hilo kwa vitu ambavyo, amedai si vya kweli.
"Mwaka 2019 tunaingia katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, nawaomba Jeshi la Polisi mkasimamie nidhamu," amesema Rais Magufuli.
Ameongeza kuwa, "Watu wasioukuwa na shukrani ndio watawasema vibaya, lakini sisi tunaotambua na kuthamini mchango wenu katika ulinzi wa taifa hili, tunatembea kifua mbele huu ni ukweli usiofichika kuwa Jeshi la Polisi mnafanya kazi nzuri".
Kwa upande wake, Inspekta Jenerali wa Polisi, IGP Simon Sirro amesema Jeshi hilo limejipanga vya kutosha kusimamia usalama katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019 na uchaguzi mkuu wa 2020, na kusema kuwa hawatatoa nafasi kwa mtu yeyote atakayehatarisha amani ya nchi.
“Tumejipanga vizuri kuhakikisha uchaguzi unakwenda vizuri. Siku zote huwa nasema kama unaamua kuchukua silaha ya AK 47 ambayo haipatikani duka lolote na kuingia nayo barabarani ili uwatishe wananchi, hatuwapi nafasi,” amesema.
Katika mahafali hayo wahitimu 513 wamemaliza kozi ya maofisa polisi na wakaguzi wasaidizi.
IGP Sirro amewataka askari hao kuhakikisha wanazingatia uadilifu katika utendaji wao kwani bila kufanya hivyo taaluma hiyo haitaleta tija kwa Taifa.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni amesema polisi hawatayumbishwa katika kusimamia amani ya nchi huku akionya maandamano yanayolenga uchochezi.
“Hatutayumbishwa, tutaendelea kusimamia amani ya nchi hii kwa mujibu wa sheria. Wale wote wanaotaka kucheza na amani ya nchi hii wakiwamo wale wanaotaka kuandamana, nasema ole wao, narudia tena ole wao,” amesema Masauni.