Jeshi la polisi mkoa wa Dodoma limefanikiwa kuwakamata watu wawili waliojifanya kuwa maafisa usalama wa Taifa waliojitambulisha kwa Mkurugenzi wa Utumishi Wizara ya Nchi ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa kutaka wapangiwe kazi idara ya elimu wakati siyo wafanyakazi.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma Gilles Muroto amesema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ,na kuwataja watu hao ni Simon Ngatunga (38) mkazi wa Makulu Dodoma,na Razin Katundu (29) mkazi wa Yombo Buza Dar-es-Salaam.
Kwa mujibu wa kamanda wa Polisi alisema kuwa Ngatunga aliwahi kuwa Mkurugenzi Halmashauri ya wilaya ya Sikonge Tabora ambaye alitumbuliwa na Rais Dkt Magufuli.
Amesema kuwa Katundu (29) alikamatwa kutokana na kitendo chake cha kutaka kusaidiwa na Ngatunga ili aweza kumfanikishia kupangiwa kazi idara ya elimu ambayo imekuwa na safari nyingi za nje ya ofisi ambapo kwa upande wake angekuwa akijipatia kipato cha ziada.
Aidha jeshi hilo linamshikilia Salum Pwao (31) mkazi wa Tabata kwa kujifanya afisa wa PSSSF anayeshughulikia mafao ya wastaafu ili waweze kulipwa mafao yao.
“Huyu Pwao amekuwa na tabia ya kuwapigia simu waastafu wanaofuatilia mafao yao na kuwadai fedha kwa ajili ya kushughulikia mafao yao hayo ili yaweze kutoka kwa haraka huku akiwadanganya pia mafaili yao yapo mezani kwake”alisema.
Kamanda huyo wa polisi katika uperesheni yake hiyo inayoendelea ikiwemo na misako alisema kuwa pia imemkamata mtuhumiwa Yona Julias (32) mkazi wa Dar-es – Salaam kwa tuhuma za utapeli wa viwanja.
Alisema mtu huyo amekuwa akiwatapeli watu mbalimbali kwa kupitia kampuni yake anayoimiloki inayofahamika kwa jina la Vijana Kwanza Project inayojihusisa na upimaji wa viwanja.
Alisema kwa kutumia utapeli wake huo ameweza kuwaibia fedha wananchi wa mikoa ya Dar-es- Slaam,Arusha na Dodoma na kuwaahidi kuwapimia viwanja na kukamilisha kisha kutokomea.
Pia jeshi hilo katika uperesheni yake hiyo limefanikiwa kuwakamata watu wawili kwa kosa la kupatikana na bhangi na misokoto 40 eneo la kikuyu katika jiji la Dodoma.
Amewataja watu hao ni pamoja na Sham Jibrea (35) na Meck Maula (40) wote wakazi wa mtaa wa Kinyambwa Kikuyu ambao watumiwa hao wamekuwa wakijihusisha na biashara ya madawa ya kulevya aina ya bhangi kwa kuwauzia wateja.
Hata hivyo kamanda huyo alitoa angalizo katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu ya Christmass na mwaka mpya madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani kwa kujiepusha na mwendo kasi.
Aidha watu wasijihusishe na uhalifu wa aina yoyote kwa kuwa uhalifu hauna nafasi na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi hili la polisi pindi wanapotilia shaka kwa vitendo vyovyote vibaya.
Social Plugin