Watu watatu wa familia moja wamefariki dunia kwa kupigwa na radi katika kijiji cha Majimaji, wilayani Tunduru, mkoani Ruvuma.
Taarifa za tukio hilo zilizothibitishwa na Mtendaji wa Kata ya Majimaji, Neema Mahujilo, zinaeleza kuwa, radi hiyo iliambatana na mvua kubwa ya upepo iliyonyesha Desemba 14, saa 12. 30 hadi saa 1.40 jioni.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Jemini Mushy, alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo na kwamba Polisi inaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo cha vifo hivyo.
Kamanda Mushy aliwataja watu waliopoteza maisha kuwa ni Zenna Hamadi Ismail (50), Yusuph Abdalah Alli (25) na Zamila Abdalah Abbilahi (3).
Mganga Msaidizi wa Hospitali ya Wilaya ya Tunduru, Edger Ngauje, aliyeifanyia uchunguzi miili ya marehemu, alisema kuwa chanzo cha vifo hivyo ni kuunguzwa na shoti ya umeme uliosababishwa na radi hiyo.