Mkazi wa Kijiji cha Nambalapi mashambani, Kata ya Masonya, wilayani Tunduru, Awetu Adam (33), amefariki dunia baada ya kupigwa na radi iliyoambatana na upepo mkali akiwa shambani.
Mvua hiyo iliyonyesha Desemba 29, mwaka huu kwa saa nne kuanzia saa 9 hadi 12 jioni imeripotiwa pia kuezua na kubomoa zaidi ya nyumba 250 za wananchi wa tarafa hiyo.
Pia imeharibu na kuvunja miundombinu ya Shirika la Ugavi Umeme Tanzania (Tanesco) kwa kung`oa baadhi ya nguzo na kusababisha ukosefu wa nishati hiyo katika baadhi ya maeneo ya mji huo.
Mbali na tukio la kifo, mtoto wa miaka miwili Bakari Said, alijeruhiwa kwa kupigwa na radi wakati akiwa amebebwa mgongoni na mama yake ambaye alikufa kwa kupigwa na radi.
Diwani wa Kata ya Mchangani, Haillu Hemed Mussa, alisema jumla ya nyumba 141, madarasa matano na ofisi za walimu katika Shule ya Msingi Mchangani, zimezuliwa.
Alifafanua kuwa pamoja na uharibifu huo pia kata yake iliripoti kujeruhiwa wananchi watatu waliotambuliwa kama, Kawale Bakari, Alli Ambe na Shekhe Mohamed Salum, ambao walikimbizwa Hospitali ya Serikali ya Wilaya kwa ajili ya matibabu.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Majengo, Abdalah Rajabu, alisema kuwa tukio la mvua hiyo limesababisha kuezuliwa kwa mapaa ya maghala mawili ya kuhifadhia korosho mali ya Chama Kikuu cha Wakulima (TAMCU) na kulowesha tani 536 za korosho, mali ya serikali.
Alisema pamoja na madhara hayo pia upepo na mvua hizo ziliezua nyumba 13 mali ya wakazi wa eneo la kata yake.
Diwani Rashid Mkwawa kutoka Kata ya Nanjoka, alisema kuwa jumla ya wakazi 11 walikosa makazi kutokana na nyumba zao kuezuliwa na mvua hizo.
Taarifa zilizotolewa na maofisa tabibu katika Hospitali ya Wilaya ya Tunduru, zinaeleza kuwa majeruhi wote wanaendelea vizuri baada ya kuanza kupatiwa matibabu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa, Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Juma Homera, alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo na tayari amewaagiza viongozi wa serikali za vijiji kuzunguka katika maeneo yao na kufanya tathmini ili kubaini hali halisi ya uharibifu huo.
Social Plugin