Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems amesema kuwa bado timu yake ina nafasi ya kusonga mbele kwenye hatua ya robo fainali ya michuano ya Klabu Bingwa barani Afrika kutokana na kundi hilo kuonekana lipo wazi kwa timu yoyote kuweza kusonga mbele.
Kocha huyo amesema hayo kupitia kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter mara baada tu Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika CAF kupanga makundi hayo ya ligi ya mabingwa na Simba kuangukia kwenye kundi D, sambamba na klabu za Al Ahaly (Misri), As Vital (Congo DRC) na JS Saoura (Algeria).
“Kundi hili lipo wazi :Michezo ya kusisimua!! … Na kiukweli tuna nafasi nzuri ya kufika robo fainali, kwa hiyo tunahitaji kuwa pamoja.”
Makundi hayo yalipangwa jana kwenye mji wa Cairo, Misri yalipo makao makuu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) ambapo Simba iliwakilishwa na mjumbe wa Bodi ya wakurugenzi wa klabu hiyo, Salim Abdallah ambapo mchezo wao wa awali wataanzia nyumbani Dhidi ya JS Saoura ya nchini Algeria.
Simba imefuzu kwenye hatua hii mara baada ya kuwatoa klabu ya Nkana FC kutoka nchini Zambia kwa jumla ya mabao 4-3 katika michezo yote miwili waliocheza nyumbani na ugenini.