VYAMA VYA UPINZANI TANZANIA VYATOA TAMKO ZITO KUHUSU DEMOKRASIA... WASEMA 2019 MWAKA WA KAZI

Vyama sita vya upinzani vilivyokaa kikao chao Zanzibar vimesema mwaka wa 2019 ni mwaka ambao watapambana kwa hali zote katika kudai haki zao wanazonyimwa kinyume na sheria za Serikali ya Jamuhuri ya Muungano ya Tanzania.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF Maalim Seif Shariff Hamad wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumaliza kikao hicho cha siku tatu kilichofanyika Zanzibar kwa niaba ya vyama hivyo.

"Kama vyama vya siasa vyenye uhalali na uratibu wa uliowekwa rasmin kikatiba, tunatangaza rasimi namna ya kufanya mikutano yetu ya hadhara katika kila kona ya nchi yetu’’ alieleza Maalim Seif.

Alieleza hawatoruhusu katazo haramu ambalo alisema linakwenda kinyume na sheria za nchi na kudai haliwezi kuzuia kazi zao.

Aliwataka wanachi pamoja wanachama wote wa vyama sita, wakati ni sasa wa kuondoa hofu na kuunga mkono vyama vyao ili kulinda Demokrasia.

"Hatupaswi kuwa waoga hata kidogo na hatupaswi kujisalimisha katika kudai haki zetu kama mtu mmoja au kikundi, lazima tupeleke ujumbe huu wa uhuru na Demokrasia kwa viongozi wenzetu wote’’ alieleza.

Sambamba na hilo waliwatangaza viongozi wa vyama vya siasa Freeman Mbowe na Esther Matiko ambao hadi sasa wako mahubusu kuwa ni Wafungwa wa kisiasa na kueleza kuwa tangazo hilo halitofutwa mpaka pale watakapoachiwa.

"Tutapambana kwa nguvu zote kuhakikisha wafungwa wote wa Kisiasa, nchi nzima wanapewa nafasi ya kupata haki katika mfumo ulio huru mbele ya mahakama na macho ya watu’’ alieleza Maalim Seif.

Mwenyekiti wa Chama cha UMMA Hashim Rungwe alisema hawawezi kumruhusu mkandamizaji wa siasa aendelee kuwakandamiza wananchi na demokrasi na kueleza sasa basi.

"Lazima tuwaeleze wananchi wakatae utawala huu wa kibabe kwani ndio uliopomorosha maisha yao’’ alifafanua Rungwe.

Alieleza kuwa Demokrasia ina gharama na wakati ukifika watawaeleza nini watafanya katika kupiga viota uvunjwaji wa Demokrasia.

Akizungumza katika mkutano huo ambao ulitoka na tamko la Azimio la Zanzibar mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia alisema hali iliyopo sasa ni kutokana na ubinafsi ya utawala uliopo.

Alieleza kuwa ubinafsi huu ndio uliopelekea maisha ya watu kubadilika na kuwaona wengine ndio walio na haki hapa nchini.

Kwa upande Wa Zanzibar vyama hivyo vilieleza kuwa hawaitambui Serikali ya Mapinduzi inayo Ongozwa Dr. Ali Muhammed Shein na kuita ni serikali haramu kutokana kile walichodai kupora ushindi wa CUF mwaka 2015.

Akizungumzia baadhi ya wabunge na Madiwani waliohama vyama na kujiunga CCM Waziri Mkuu wa zamani Fredric Sumaye alieleza kuwa viongozi hao hawakuhama bure na wameenda kufanya biashara ya kisiasa.

"Unapoona wabunge na viongozi wa upinzani wanahamia chama tawala ujue chama tawala kimefika mwisho kutawala katika nchi, na hapa ni dhahiri CCM wamefikia mwisho kutawala Tanzania’’ alieleza Sumaye

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم