Mmoja wa Watumishi wa TASAF,Shadrack Mziray akiwasilisha taarifa kwenye Mkutano wa Wadau ,serikali na TASAF jijini Dar es salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF ,Bw. Ladslaus Mwamanga (katikati) akiongoza mkutano wa Wadau wa Maendeleo, Maafisa wa Serikali na TASAF kwenye ukumbi wa Mfuko huo jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Washiriki wa Mkutano wa Wadau ,Serikali na TASAF wakiwa kwenye ukumbi wa Mikutano wa TASAF jijini DSM katika mkutano uliojadili utekelezaji wa Shughuli za Mfuko huo na maandalizi ya awamu ya pili ya Mpango huo inayotarajiwa kuanza hapo mwakani.
Picha ya juu na chini menejimenti ya TASAF na ile ya Benki ya Dunia hapa nchini wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watumishi wa TASAF, Serikali Na Wadau wa Maendeleo baada kuhudhuria mkutano wao wa pamoja jijini Dar es salaam.
***
Na Estom Sanga-DSM
Mkutano wa Wadau wa Maendeleo ,Maafisa wa Serikali na Watendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF uliojadili kwa kina utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ambao unatekelezwa na Serikali kupitia TASAF umemalizika jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo ambao hufanyika kila baada ya miezi sita , umefanyika kufuatia ziara ya washiriki hao katika wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza na Unguja ambako walikutana na Walengwa wa Mpango huo na kujionea namna Walengwa wanavyoendelea kunufaika na huduma zinazotolewa na Mpango huo kuboresha maisha yao.
Miongoni mwa mambo yaliyofanywa katika mkutano huo ni pamoja na kuweka mkakati wa utekelezaji wa awamu ya pili ya Mpangowa Kunusuru Kaya Maskini inayotarajiwa kuanza Mwezi Aprili hapo mwakani ambayo italenga zaidi katika kuwashirikisha Walengwa kufanyakazi za maendeleo kwenye maeneo yao na kisha kulipwa ujira.
Akizungumza na Washiriki wa Mkutano huo Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF,Bw. Ladislaus Mwamanga ametoa wito maalumu kwa wadau na maafisa wa Mfuko huo kufanya kazi kwa bidii na kuweka mbele maslahi ya taifa ili lengo la serikali la kuwapunguzia kero ya umaskini wananchi liweze kufikiwa kwa ufanisi.
Bwana Mwamanga amesema utekelezaji na mafanikio ya Mpango huo unategemea kwa kiwango kikubwa jitihada za pamoja hasa ikizingatiwa kuwa wananchi wanaolengwa ni wale ambao kwa kiwango kikubwa wamekuwa wakiishi katika hali ya umaskinina wengine kukata tamaa jambo ambalo amesema linapaswa kukabiliwa kwa nguvu za pamoja.
Kwa upande wake Kiongozi wa shughuli za TASAF katika Benki ya Dunia hapa nchini Bwana Mohamed Muderis amepongezea jitihada za dhati zinazofanywa na Watumishi wa TASAF na wadau wengine katika kuwahudumia Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na hivyo kuleta hamasa ya dhati ya Walengwa kuuchukia umaskini.
Aidha Bwana Muderis ametoa rai kwa watumishi hao kuendelea na kukamilisha kwa wakati maandalizi ya sehemu ya pili ya Mpango wa kunusuru kaya maskini inayotarajiwa kuanza mapema mwakani na kuzingatia kwa dhati maelekezo ya serikali .
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii –TASAF upo kwenye maandalizi ya sehemu ya pili ya Mpango wa kunusuru Kaya Maskini baada ya kukamilika kwa sehemu ya kwanza huku mkazo ukiwekwa kuwawezesha walengwa kushiriki katika kazi za Ajira ya Muda, kuunda vikundi vya kuweka akiba na kukopeshana,ujenzi wa miundombinu hasa katika sekta za elimu, afya ,maji na kuanzisha shughuli za uzalishaji mali ili kujiongezea kipato.
Social Plugin