Na Humphrey Shao, Globu ya Jamiii
Baada ya kurasimishwa kwa iliyokuwa bandari bubu ya Bagamoyo Mamlaka ya Mapato Tanzania imeongeza kiasi cha makusanyanyo yake hadi kufikia bilioni 1.2 kwa mwezi huku mamlaka ya usimamizi bandari TPA ikiingiza hadi sh milioni 33 kwa siku kutoka sh 600,000.
Hayo yameelezwa jana na Msimamizi wa bandari hiyo kwa upande wa TPA, Withara Jared Withara, wakati akizungumza na waandishi wa habari bandarini hapo kuhusiana na hatua walizopiga baada ya kurasimishwa na mpango uliopo wa kufanya maboresho ya bandari hiyo.
Alisema mapato hayo yanatokana na usafirishaji wa bidhaa kwenda na kutoka visiwa vya Zanzibar ambao hufanywa kwa kutumia majahazi ambapo kwa siku moja huweza kuhudumia hadi majahazi nane na shehena tani 1000.
Alitaja bidhaa zinazosafirishwa sana katika bandari hiyo kuwa ni mafuta ya kula, mbao, kokoto, vilainishi vya mashine pamoja na mazao ya chakula kama vile vitunguu, nyanya, hoho n.k. “na bidhaa nyingi zinatoka Zanzibar kuja bara kuliko zile zinazoenda kule kutoka huku.”
Akielezea historia ya bandari hiyo alisema ilianzishwa toka enzi za biashara ya utumwa mwaka 1892 baada ya utumwa kukomeshwa ilikuwa ikitumika kama bandari bubu na baadae ikiwa inasimamiwa na TRA kitengo cha forodha hadi mwaka 2009 ilipochukuliwa na TPA.
Kuhusu mpango wa maboresho ya bandari hiyo alisema kuna mpango wa kujenga ukingo kuzuia mmomonyoko pamoja na kuboresha gati iliyopo ambayo ni ya mda mrefu pamoja na kununua boti ya kufanya ulinzi ili kuzuia bandari bubu zinazozunguka bandari hiyo.
"Uwepo wa bandari bubu unapunguza majahazi yanayokuja kwenye bandari yetu na hivyo kupoteza mapato na kuhatarisha usalama wa nchi na wananchi kwasababu vitu vinaingizwa kimagendo," alisema Withara.
Mpango wa kufufua bandari bubu ambazo zipo zaidi ya 250 nchi nzima utaongeza mapato ya mamlaka kwa kiasi kikubwa sambamba na kudhibiti bidhaa za magendo nchini.
Inakadiriwa kuwa jumla ya mapato ya bandari hizo yanaweza kufikia theluthi moja au nusu ya mapato ya Bandari ya Dar es Salaam.
Bandari ya Dar es Salaam ambayo imefikia kuhudumia shehena za tani milioni 16.2 kwa mwaka inaingiza Sh bilioni 70 kwa mwaka kwa mujibu wa takwimu za TPA za mwaka 2017.
Zipo hatua kadhaa zinazochukuliwa katika mpango wa kufufua bandari bubu ikiwemo kuzianisha, kuwashirikisha wadau, kuzifanyia tathmini, kuandika ripoti ya kuanisha bandari zenye sifa za kuweza kufufuliwa na kisha kuipeleka kwa wizara husika kwaajili ya mapitio na kupitishwa.
Kwa sasa zoezi la kuzitambua na kuzianisha zinaendelea na kwa mujibu wa TPA zoezi hilo linatarajia mwezi huu na kwamba likikamilika zinaweza kufikia bandari bubu zaidi ya 300."
Tayari vikao vimeshafanyikakati ya TPA na wakuu wote wa mikoa na wilaya ambazo zina bandari bubu na nusu ya viongozi wote wa vijiji na kata katika maeneo hayo tayari wameshashirikishwa kwenye suala hilo na vikao vinaendelea.
Ushirikishwaji huo wa wadau umefanyika ili kupata ushirikiano katika utekelezaji wa usimamizi wa bandari hizo pindi zitakaporasimishwa na kutopata mapingamizi.
Hatua hii ni miongoni mwa mabadiliko makubwa yanayofanywa na TPA katika kuhakikisha bandari zinachangia kwa kiasi kikubwq ukuaji wa uchumi wa taifa.
Msimamizi wa Bandari ya Bagamoyo Withara Jared Withara, akizungumza na Waandishi wa Habari namna bandari hiyoilivyochangia katika kuongeza mapato.
Mmoja wa Wachuuzi katika Mwalo wa Bandari ya Bagamoyo akipita na Biashara yake ya Miwa
Jahazi likipakia shehena ya Mbao kwa ajili yakupeleka katika Visiwa vya zanzibar kama ilivyokutw ana Mpiga picha wetu aliyetembelea banadari hiyo ambayo kwa sasa Imerasimishwa.
Mmoja ya wavuvi wa Samaki akiwa amebeba ndoo zake za Samaki akielekea nazo katika soko la Samaki katika eneo la Bandari ya Bagamoyo
Korido ya Bandari ya Bagamoyo kama ainavyoonekana pichani uku shughuli za kibinadamu zikiendelea.