Katika hali isiyokuwa ya kawaida mtoto anayekadiriwa kuwa na umri wa miezi mitano, jijini Dodoma amefungiwa kabatini na mwajiri wa mama mzazi wa mtoto huyo ambaye alikuwa akifanya kazi za ndani.
Akithibitisha kupokelewa kwa mtoto huyo katika hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo Dkt. Ibenzi amesema kuwa mtoto amefikishwa hospitali siku tatu zilizopita na kwamba atatibiwa kwanza tatizo la ukosefu wa lishe (utapiamlo).
Dkt. Ibenzi amesema kuwa mama wa mtoto huyo alifikishwa hospitalini hapo akiwa hajitambui kwa kile kilichodaiwa kupigwa na mwajiri wake hadi kupoteza fahamu.
"Mtoto anaendelea na matibabu kwakuwa bado tunamfanyia uchunguzi zaidi ikiwemo kufuatilia kama alipotiwa chanjo zote stahiki, na sisi tunatibu wagonjwa tu, mambo mengine watayafuatilia wahusika", amesema Dkt. Ibenzi.
Taarifa za awali zinadai kuwa binti huyo alipata ujauzito akiwa nyumbani kwa mwajiri wake anayedaiwa kuwa ni mwalimu wa shule ya msingi jijini humo ambaye alimtaka kufanya siri ili majirani wasifahamu kama yeye ni mjamzito.
Baadaye alifanikiwa kujifungua na kuendelea kufanya siri na mtoto kuhifadhiwa kabatini, hadi hapo juzi ambapo inadaiwa alimpiga binti huyo hadi kupoteza fahamu ndipo majirani walipofika eneo la tukio na kugundua kulikuwa na mtoto mchanga ndani ya kabati.
Chanzo:Eatv
Social Plugin