Jeshi la Polisi nchini, limeelezea kuchukizwa na ujumbe wa video unaoendelea kusambazwa unaomwonyesha askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani akipokea rushwa.
Mkuu wa Jeshi hilo, Inspekta Jenerali (IGP) Simon Sirro, ametoa onyo kali kwa raia wanaosambaza tukio hilo la zamani na kusema lengo la wahusika ni kudhalilisha jeshi hilo.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa Jeshi hilo Makao Makuu ya Polisi, Naibu Kamishna (DCP) Ahmed Msangi, ilisema tukio hilo lilitokea Novemba, 2016 eneo la Kabuku mkoani Tanga.
IGP Sirro alisema askari anayeonekana kwenye video hiyo alichukuliwa hatua za kinidhamu kwa kufukuzwa kazi na taratibu zingine za kisheria kufuatwa.
Aidha, alisema katika siku za karibuni kumeibuka kikundi cha watu wanaosambaza video inayomwonyesha askari huyo akipokea fedha kutoka kwa dereva wa gari dogo.
Aliwataka wananchi kuacha kusambaza video hiyo yenye lengo la kulichafua Jeshi la Polisi hasa Kikosi cha Usalama Barabarani.
“Tayari uchunguzi wa kuwabaini waliosambaza umeshaanza na yeyote atakayebainika kuhusika kusambaa kwa video hii atachukuliwa hatua za kisheria,” alisema Sirro.
Aliwataka wananchi wote kuacha kutumia vibaya mitandao ya kijamii badala yake waitumia kupeana taarifa zinazochangia kuleta maendeleo nchini.
IGP Sirro alisema Jeshi la Polisi linazingatia weledi katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zinazoliongoza.
“Wananchi endeleeni kushirikiana na Jeshi la Polisi katika vita dhidi ya uhalifu kwa kutoa taarifa za wahalifu na uhalifu,” alisema IGP kwenye taarifa hiyo.