Aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) sasa TRC, Kipallo Kisamfu na wenzake 17 wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka 15 ya matumizi mabaya ya madaraka.
Kisamfu na wenzake ambao ni wahandisi na mameneja walipandishwa kizimbani jana Jumatano Desemba12, 2018 kwa kuingia mikataba ya zabuni ya ununuzi wa vichwa vya treni na kuipa zabuni hiyo kampuni ya Hindusthan Engineering and Industries Limited
Hayo yalielezwa na mwendesha mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Maghela Ndimbo mbele ya HakimuMkazi Mkuu, Wilbroad Mashauri
Mbali na Kisamfu washtakiwa wengine ni Gilbert Alfred Minja ambaye alisomewa mashtaka bila kuwepo mahakamani pamoja na Paschal John Mafikiri (Kaimu mhandisi mitambo mkuu).
Wengine ni Anthony Emmanuel Munishi (meneja usambazaji) Charles Ndenge (kaimu meneja wa usafirishaji), Ferdinand Soka (kaimu meneja msaidizi wa usambazaji), Muungano Kaupunda (kaimu mkuu wa kitengo cha ufundi).
Joseph Syaizyagi, Kedmond Mapunda, Lowland Simtengu, Ngoso Ngosomwile, Yonah Shija, Malumbo Malumbo, Stephan Kavombwe, Donatus Bandebe, John Charles na Ally Mwangila.
Katika shtaka la kwanza dhidi ya aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa TRL, Kipallo Kisamfu inadaiwa Machi 21 mwaka 2013 huko katika makao makuu ya kampuni hiyo, alitumia madaraka yake vibaya kwa kusaini mkataba wa zabuni kwa Kampuni ya Hindusthan Engeering and Industries Limited bila kuhakiki mkataba huo utatekelezeka kwa kuzingatia masharti ya mkataba.
Aidha imedaiwa, Kaimu Mhandisi Mkuu wa Ufundi, Paschal Mafikiri, anadaiwa kati ya Februari 21 na Agosti 15 mwaka 2013 alishindwa kutoa taarifa ya mkataba wa zabuni wa kampuni hiyo na kusababisha Kampuni hiyo ijipatie manufaa.
Pia inadaiwa, Mafikiri aliidhinisha michoro 274 ya mabehewa ya mizigo kwa Kampuni ya Hindusthan kinyume na mkataba wa zabuni.
Mshtakiwa huyo pia anadaiwa kwamba kinyume na mkataba aliidhinisha michoro ya mabehewa iliyoandaliwa na Kampuni ya Hindusthan.
Aidha mshtakiwa Kaupunda, kiwa Kaimu Mhandisi wa Ufundi na Mkuu wa Idara anadaiwa Kuidhinisha mchoro wa mabehewa na mafuta iliyoandaliwa na kampuni hiyo.
Pia, washtakiwa, Kaupunda, Syaizyagi, Mapunda na Simtengu wanadaiwa kati ya Januari 10 na Februari 20 wakiwa waajiriwa wa TRL kwa nafasi zao za Mhandisi Mkuu wa Ufundi, Mchoraji Mkuu na Msaidizi Mkuu wa Meneja wa Usafirishaji wa Reli na wote wajumbe Kamati ya uthamini walitumia madaraka vibaya kwa kushindwa kufanya uchambuzi za zabuni.
Shtaka la saba kwa mshtakiwa Munishi , Meneja Mkuu wa Usambazaji, anadaiwa kuidhinisha usambazaji wa mabehewa 274 Febriaro11,2013 bila kuwasilisha ripoti hiyo kwenye bodi ya zabuni .
Washtakiwa Minja, Mafikiri, Massae, Munishi na Ndenge, wanadaiwa Februari 20,2013 kwa kutumia madaraka yao vibaya waliidhinisha mapendekezo ya kamati ya uthamini katika mkataba wa Kampuni ya Hindusthan kusambaza mabehewa 274 .
Aidha, mshtakiwa Ngosomwiles, anadaiwa Aprili 10 mwaka 2014 huko Katika maeneo ya karakana ya Tiljala India akiwa Kaimu Mhandisi Mkuu wa Ufundi alitumia madaraka vibaya kwa kuidhinisha uzalishaji wa mabehewa 50 bila kufuata masharti
Wakili Ndimbo amedai mshtakiwa Shija na Malumbo, wanashtakiwa kwamba Julai 16,2014 waliidhinisha Kampuni ya Hindusthan kuzalisha mabehewa 174 ya mizigo na shtaka la 11 linamkabili Kavombwe na Bandebe wanadaiwa Septemba 4,2014 huko Santragachi India waliidhinisha kampuni hiyo kuzalisha mabehewa 50 ya matanki ya mafuta Shija na Malumbo wanadaiwa Julai 17,2014 waliidhinisha kusafirishwa kwa mabehewa 50, Pia mshtakiwa Kavombwe na Bandebe wanadaiwa kuidhinisha kusafirishwa kwa mabehewa 174 kuingia nchini bila kufuata masharti ya mkataba .
Pia washtakiwa Charles na Mwangila wanadaiwa kati ya Aprili 26 na 27 mwaka 2015 walitumia vibaya kwa kuidhinisha Kampuni ya Hindusthan kuingiza nchini mabehewa 50 ya mafuta na 27 ya mizigo bila kuwa na uhakika kwamba mkataba utatekelezeka .
Washtakiwa wote walikana mashtaka yao na wako nje kwa dhamana hadi Januari 18 kesi itakapotajwa. Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelekezi katika kesi hiyo bado haujakamilika
Social Plugin