VYAMA 10 WA UPINZANI TANZANIA VYACHACHAMAA

Vyama 10 vya upinzani nchini Tanzania vimemtaka Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kurejesha ratiba za vikao vya Baraza la Vyama vya Siasa ili kupata fursa ya kujadili Muswada wa Marekebisho ya Vyama vya Siasa kabla ya kuanza kwa vikao vya kamati za Bunge.

Akisoma tamko la vyama hivyo, leo Jumamosi Desemba 22, 2018 jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Salum Mwalimu amesema kuwa Msajili na ofisi yake wana nia ya kuvuruga kikao hicho ambacho walikubaliana kuketi Desemba 21 na 22, 2018 kabla ya kikao kijacho cha Bunge.

Mwalimu amesema wameshtushwa na uamuzi wa Msajili kwa kile wanachokidai kuahirisha kikao hicho na kukwamisha lengo lao la kujiandaa kutumia fursa hiyo kuzungumzia muswada ambao wamedai kuwa ni kandamizi na usiofaa.

"Tumeshtushwa kwanza na utaratibu uliotumika wa kuahirisha kikao ambacho tayari kilishakuwa kimepangwa na Kamati ya Uongozi ya Baraza la Vyama vya Siasa ambalo ndilo lenye jukumu la kikao chake," amesema.

"Tunataka Jaji Mutungi aseme amemshirikisha nani kufanya uamuzi huo, mwenyekiti wetu wa baraza ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya uongozi hakuwa na hiyo taarifa ya ahirisho la hicho kikao, " ameongeza.

Moja ya vifungu vinavyopendekezwa kufanyiwa marekebisho ni kifungu cha 19, ambacho kinapendekeza kurekebishwa ili kumwezesha msajili wa vyama vya siasa kufuta usajili wa chama cha siasa kitakachobainika kupata usajili kwa njia zisizo za halali.

Muswada pia unapendekeza kufuta kifungu cha 21A na kifungu cha 21B kinapendekezwa kufanyiwa marekebisho ili kuliwezesha Baraza la Vyama vya Siasa kupata fedha kutoka katika bajeti ya Serikali na wafadhili.

Pia, inapendekeza kufanyiwa marekebisho ili kumpa mamlaka waziri mwenye mamlaka ya kutengeneza kanuni za uandaaji wa taarifa za hesabu za vyama vya siasa na mambo yatakayojumuishwa katika katiba za vyama vya siasa.

Muswada huo umesomwa kwa mara ya kwanza bungeni ambako Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge alisema Spika wa Bunge, Job Ndugai ataipangia Kamati ya Bunge itakayofanya uchambuzi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post