Wananchi wa vitongoji vilivyopo kijiji cha Muungano, wilayani Momba, wameyakimbia makazi yao wakihofia kukamatwa baada ya kuwapo kwa msako wa kuwakamata wasiokuwa na vyoo.
Kata ya Kamsamba ni miongoni mwa kata wilayani Momba ambayo imekumbwa na ugonjwa wa Kipindupindu na watu zaidi ya 100 kuugua na kusababisha serikali kuweka mikakati ya kudhibiti ugonjwa huo.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kamsamba, Gerad Makwasa, alisema viongozi ngazi ya wilaya wakiwa na askari mgambo, walifika katika bonde la Kamsamba kuendesha doria kuwasaka wasiokuwa na vyoo, hali iliyowalazimu wakazi wa kijiji hicho kukimbilia kusikojulikana.
Ofisa Tarafa ya Kamsamba, Zakayo Mwasomola, alisema juzi walikaa kikao na Mganga Mfawidhi wa kituo cha afya cha Kamsamba kujadili hali hiyo ambapo alisema kata zilizokumbwa zaidi ni ugonjwa huo ni Ivuna wagonjwa 35, Samang’ombe 35 na Kamsamba 34 na aliyefariki dunia ni mmoja.
Alisema ugonjwa huo uliibuka Novemba 11 mwaka huu na jitihada zinafanyika kudhibiti hali hiyo.
Alisema wamekuwa wakihamasisha watu kuweka hali ya usafi wa mazingira,kujenga vyoo bora,kuchemsha maji ya kunywa na kunawa kwa sabuni pindi watokapo chooni.
“Ni kweli wananchi karibu wote wa kijiji cha Muungano wameyakimbia makazi yao wakihofia kukamatwa, lakini tumeandika majina yao, tunafahamu kuwa watarejea tu kwani wameacha familia zao wengine wake zao ni wajawazito,’’alisema Mwasomola.
Mwenyekiti wa kamati ya Maafa,Juma Irando, alisema hiyo ni
operesheni endelevu ya kuhakikisha kila kaya inakuwa na choo bora ambacho kitakuwa kinatumika.
Irando ambaye pia ni Mkuu wa wilaya hiyo, alisema kata hiyo imekumbwa na Kipindupindu kutokana na watu wengi kutokuwa na vyoo na walitoa muda wa kujenga kwa hiyari kuanzia Novemba 30 mwaka huu hadi Desemba 30 mwaka huu.
Alisema huo ulikuwa ni mkakati wa kimkoa ambapo tayari
siku zimekwisha na sasa wapo katika utekelezaji.
Alisema kwamba kitendo cha wanakijiji hao kukimbia sio dawa ya kumaliza tatizo, kwani operesheni hiyo ni endelevu.
Social Plugin