Rais Magufuli amelazimika kuingilia kati sakata la kutotambuliwa kwa wafanyabiashara wadogo nchini kwa kuchapisha vitambulisho maalum kwa ajili ya kuwatambua wafanyabiashara hao ili waweze kufanya kazi zao kwa uhuru.
Rais Magufuli ametoa uamuzi huo wakati akizungumza na Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Mamlaka ya Mapato ya Tanzania TRA pamoja na Wakuu wa Wilaya kwenye mkutano wa pamoja kujadili namna ya kufikia malengo ya ukusanyaji wa mapato kwa mwaka wa fedha 2018/2019..
"Nimeamua kufanya tofauti, nimeamua kuchapisha vitambulisho mimi mwenyewe, na hivi vitambulisho vina alama ya siri na vitaanza kuanzia namba moja, kitambulisho kimetolewa na ofisi ya Rais Tamisemi kwa ajili ya matumizi ya TRA, na kwa kuwa nakitoa mimi hakuna mtu wakumsumbua mmachinga."
Aidha Rais Magufuli amesema vitambulisho hivyo watakabidhiwa wakuu wote wa mikoa nchini ambapo kila mmoja atapatiwa jumla ya vitambulisho elfu 25 kwa ajili ya kuwakabidhi wafanyabiashara wadogo kwenye Mkoa wake.
Awali katika mkutano huo, Rais Magufuli amezungumzia kuhusu suala la utozaji kodi za nyumba, "mfano kodi ya majengo ni kubwa sana, majengo yaliyosajiliwa mpaka sasa ni milioni 1.6 napenda kurudia kodi ya majengo iwe shilingi elfu 10 kwa nyumba ya kawaida, na shilingi 20 kwa nyumba za juu na shilingi elfu 50 kwa nyumba za mjini, zitozwe kulingana na hati ya kiwanja, na si idadi ya nyumba kwenye kiwanja".
Chanzo -EATV
Social Plugin