Zaidi ya wanafunzi 4,000 waliohitimu darasa la saba mwaka huu na kufaulu, wako hatarini kukosa fursa ya kujiunga na kidato cha kwanza hapo mwakani kutokana na upungufu
Mbunge wa Jimbo la Ilemela ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula aliyasema hayo jana wakati akipokea mifuko 100 ya saruji kutoka benki ya Diamond Trust (DTB).
Dkt. Mabula alisema wanafunzi 8,350 wamefaulu mtihani wao wa darasa la saba lakini kuna upungufu wa vyumba 84 vya madarasa hivyo wenye uhakika wa kujiunga na elimu ya kidato cha kwanza ni wanafunzi takribani 4080. Wilaya ya Ilemela ilishika nafasi ya kwanza kwa ufaulu mkoani Mwanza na kitaifa nafasi ya sita.
Hivyo Dkt. Mabula alisema mifuko hiyo ya saruji kupitia taasisi yake ya The Angeline Foundation inayoshirikiana vyema na Halmashauri ya Ilemela, itasaidia kufyatua matofali kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa ili kuhakikisha wanafunzi waliofaulu wanapata nafasi ya kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza ambapo aliwahimiza wadau wengine kuunga mkono juhudi hizo.
Naye Meneja wa DTB Tawi Kuu la Mwanza, Nabeel Alnoor alisema benki hiyo itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kuchangia shughuli mbalimbali za maendeleo ya kijamii katika Mkoa Mwanza hususani katika sekta ya elimu na afya.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Kutoka kushoto ni Meneja Msaidizi DTB Tawi Kuu la Mwanza, Ezra Shandu, Meneja DTB Tawi Kuu la Mwanza, Nabeel Alnoor, Mbunge jimbo la Ilemela, Dkt. Angeline Mabula pamoja na Afisa Masoko DTB Tawi Kuu la Mwanza, Boniphace Mwita.
Mbunge jimbo la Ilemela, Dkt. Angeline Mabula akishiriki zoezi la kupanda miti iliyotolewa na Benki ya "DTB" katika Shule ya Msingi Kitangiri C.
Mbunge jimbo la Ilemela, Dkt. Angeline Mabula (wa pili kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Meneja Msaidizi DTB Tawi Kuu la Mwanza, Ezra Shandu (kushoto), Meneja DTB Tawi Kuu la Mwanza, Nabeel Alnoor ( wa pili kulia) na Afisa Masoko DTB Tawi Kuu la Mwanza, Boniphace Mwita (kulia).
Tazama BMG Online TV hapa chini
Social Plugin