Jessica Hayes alijinunulia mwenyewe shela, ushungi na pete ya ndoa. Lakini aliposimama altareni kufungishwa ndoa na Askofu, hakuwepo bwana harusi pembeni yake.
Bi Hayes, 41, ni mwanamke bikra aliyejihifadhi ili awe mke wa Mungu. Hii ni ada ambayo si ya lazima wanayoweza kufanya wanawake wanaoamini katika ukatoliki kwa kujitoa wakfu miili yao kwa Bwana kwa maisha yao yote.
Lakini hata ndani ya Ukatoliki, ada hii inayofahamika kwa kingereza kama consecrated virgins si maarufu- na waumini wachache wanafahamu juu ya mabikra hao- moja ya sababu ni kuwa ada hiyo iliruhusiwa kwa uwazi na kanisa chini ya miaka 50 iliyopita.
Katika sherehe ya wakfu ama harusi, mwanamke bikra ambaye huvaa shela jeupe- hula kiapo cha maisha cha kutojihusisha na mahusiano ya kimapenzi na kutokufanya ngono.
Wanawake hao pia huvaa pete za ndoa - ambayo huwa ni alama ya kufunga uchumba ama ndoa na Kristo.
"Mara nyingi naulizwa: 'Kwa hiyo, umeolewa?'" anasema bi Hayes. "Kawaida huwajibu kuwa mimi ni sawa tu na wanawake watawa (masista) wa kanisa, na nimejitoa kwa Kristo kwa moyo wote, tofauti mie naishi nje na watu wa kawaida."
Chanzo:Bbc
Social Plugin