Waziri wa Nishati Dr. Medard Kalemani ameagiza kuchukuliwa kwa hatua za kinidhamu ikiwemo kuwavua nyadhifa zao manaibu Wakurugenzi wa sekta ya uzalishaji na usambazaji wa Shirika la umeme nchini (TANESCO) kutokana na uzembe uliojitokeza kwenye gridi ya taifa na kusababisha umeme kukatika mara kwa mara nchi nzima.
Akizungumza jana jioni Jumamosi Desemba 15, 2018 baada ya kukutana kwa dharura na bodi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Kalemani alisema katika kipindi cha miezi miwili Gridi ya Taifa imetoka mara nne kuanzia Novemba 28 hadi Desemba 14, 2018.
Alisema kitendo hicho ni hatari kwa usalama wa Taifa ikizingatiwa kuwa nchi ina ziada ya umeme wa wastani wa megawati 252
Alisema nchi inapokuwa gizani hata kwa sekunde moja maana yake hakuna usalama na kutoa maelekezo kwa bodi hiyo kuchukua hatua.
“Lazima kuchukua hatua kuhakikisha hilo halijitokezi. Mwenyekiti (wa bodi) unda timu mahsusi kuanzia leo ya kuchunguza na kufuatilia jambo hilo kwa kushirikisha tasnia na taasisi mbalimbali si Tanesco pekee.
“Ndani ya siku saba nipate matokeo ya nini chanzo cha tatizo hilo ili lisijirudie kabisa. Jambo hili linapotokea ina maana kuna uzembe katika usimamizi ama kutofuatilia a maagizo ya Serikali.” Alisema
Social Plugin