Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora, Kapteni mstaafu George Mkuchika, amewashangaa wakuu wa mikoa na wilaya wanaoweka watu ndani saa 48 na kusema katika kipindi chake cha miaka 22 alichokuwa mkuu wa mkoa na wilaya hajawahi kumweka mtu ndani.
Aidha, alisema anajivunia kuwa Mtanzania aliyeteuliwa na marais watano nchini kushika nyadhifa mbalimbali ikiwamo za ukuu wa mkoa na wilaya.
Mkuchika alitoa kauli hiyo jana kwenye mafunzo ya Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa ya Tanzania Bara yaliyoandaliwa na Taasisi ya Uongozi, jijini hapa.
Akielezea jinsi alivyoteuliwa katika vipindi vya marais watano, alisema hayati Baba wa Taifa Julius Nyerere, alimteua kuwa mkuu wa wilaya akiwa na umri wa miaka 35, Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, alimteua kuwa mkuu wa wilaya na Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa alimteua kuwa mkuu wa mkoa.
"Rais mstaafu Jakaya Kikwete yeye alinipa uwaziri, Rais John Magufuli amenipa uwaziri sasa namngoja Rais wa awamu ya sita," alisema.
Aliongeza: "Mimi naitwa Waziri wa Utawala Bora sina mipaka, wewe mkuu wa wilaya umepewa mamlaka ya kumweka mtu saa 24 au 48, napiga simu kwa bosi wako kwa kuwa umetumia madaraka yako vibaya akikupeleka mahakamani unashtakiwa."
Alisema serikali inaendeshwa kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni, hakuna mtu anayeweza kuendesha bila kujua hizo sheria zinasemaje.
Alisema baada ya wakuu wa wilaya kupata mafunzo, figisu figisu za kuweka watu ndani zimepungua.
"Mimi nimekuwa DC (Mkuu wa Wilaya) miaka 14, nimekuwa mkuu wa mkoa miaka minane, sijawahi kuweka mtu ndani hata siku moja."
"Sheria inasema unamuweka mtu ndani kwa usalama wake kama ameua, ndugu wa marehemu wanataka kulipiza kisasi unaenda kumficha ndani, sasa mtu kachelewa kwenye mkutano wa DC au RC unamuweka ndani wakati zipo taratibu za kushughulika naye," alihoji.
Alisisitiza serikali kuendeshwa kwa kutumia sheria, taratibu na kanuni.
"Nataka kusisitiza muendesha serikali kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni," alisema.
Aidha, alisema waziri kufunga safari bila kutoa taarifa kwa mkuu wa mkoa mahali anapokwenda ni kosa.
"Ningekuwa mimi mkuu wa mkoa ningepeleka polisi kwenda kublock kwa kuwa mimi sina taarifa na ugeni huu, lakini na mimi nimefanya hiyo kazi kuna wengine wagumu, taratibu za kiserikali zinataka waziri unapokwenda kutembelea kwenye mkoa unatuma taarifa," alisema.