Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, amesema kuna baadhi ya watumishi na viongozi serikalini wana roho mbaya kama nyoka.
Amesema kuna baadhi ya watumishi ambao wamekuwa wakijijali wenyewe kuliko watumishi walioko chini yao na kusisitiza kuwa kama wapo katika wizara yake washindwe na walegee.
Aliyasema hayo juzi wakati wa utoaji tuzo ya utumishi iliyotukuka kwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mussa Iyombe, iliyotolewa na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (Jica).
“Tuwe na upendo, tusiwe na tabia ya nyoka, maana nyoka namfahamu hata akiwa mfupi au mrefu lakini roho yake mbaya atamgonga nyati, kumla hawezi lakini basi tu,” alisema Jafo na kusababisha watu kuangua kicheko.
Jafo alisema kuna baadhi ya watumishi wanafanya mambo ya aibu na kuna baadhi ya mabosi wanaposafiri na madareva wao kwenda mikoani, wanakaa na pesa za mafuta badala ya kuwakabidhi madereva.
Alisema pindi mafuta yanapoisha mabosi hao ndipo wanatoa pesa na kuwapa madereva, lakini jambo la kushangaza wakati wa kufanya marejesho ya pesa madereva ndio wanahusika.
Social Plugin