Mjumbe wa Baraza la wadhamini la klabu ya Yanga, Mama Fatma Karume amewataka viongozi wa Yanga kuahakikisha wanafanya uchaguzi bila kuiogmbanisha Yanga na serikali kwa maslahi yao binafsi.
Akiongea na baadhi ya wanachama wa Yanga kuhusu mwenendo wa klabu hiyo, Mama Fatma Karume alieleza kushangazwa na maneno yanayoenezwa kuwa huenda uchaguzi wao unakwamishwa na serikali kupitia BMT jambo ambalo si kweli.
''Hizi chokochoko zinatoka wapi, mara uchaguzi usifanyike kwa kusingizia serikali inaingilia, niwaombe tufanye uchaguzi vizuri hawa viongozi wenye kuigombanisha Yanga na serikali hatuwahitaji'' , amesema.
Mbali na hilo Mama Fatma amewahakikishia wanachama wa Yanga kuwa serikali haiwezi kuingilia uchaguzi wao endapo watafuata taratibu zote kwa mujibu wa sheria na katiba ya klabu hiyo pamoja na maelekezo mengine kutoka TFF na mamlaka zinazohusika.
''Serikali yetu ni makini na inasimamia kila lililojema, kwahiyo tuipende na tusitake kuifitinisha na Yanga, Yanga tunaipenda na serikali yetu tunaipenda tufuate taratibu ili timu yetu ipate viongozi wanaofaa'', ameongeza.
Yanga ipo kwenye sintofahamu juu ya suala la uchaguzi wao ambao unasimamiwa na kamati ya uchaguzi ya TFF lakini wao kama klabu wamekuwa wakishinikiza uchaguzi huo usiguse nafasi ya mwenyekiti jambo ambalo TFF hawaliungi mkono.
Social Plugin