Baada ya kufanikiwa kuibuka na ushindi dhidi ya Mbeya City jumla ya mabao 2-1 hapo jana katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, wadau wa klabu ya Yanga wamechanga kiasi cha Sh. 960,000 kuwapongeza wachezaji kwa ushindi.
Mashabiki hao kutoka Wilaya ya Mbozi wakiongozwa na waziri wa kilimo Japhet Hasunga pamoja na mkuu wa mkoa wa Lindi Erasto Zambi wamechangia kiasi hicho cha pesa kama motisha kwa wachezaji pamoja na benchi la ufundi kutokana na kushinda mchezo huo.
Wadau hao wachache waliamua kuchangishana fedha kutoka mifukoni mwao ambazo waliwagawia kiasi cha Sh 35,000 kila mchezaji na Sh 30,000 kwa kila mmoja katika benchi la ufundi la klabu hiyo kama shukurani zao kwa kuwafanya mashabiki wao kufunga mwaka kwa furaha.
Yanga inaongoza ligi mpaka sasa ikiwa na jumla ya pointi 50 baada ya kushuka dimbani michezo 18, ikimuacha mpinzani wake Azam FC aliye katika nafasi ya pili kwa tofauti ya pointi 10.
Pia imeweka rekodi ya kutopoteza mchezo wowote mpaka sasa, ikiwa imeshinda michezo 15 na kwenda sare michezo miwili, huku ikiondoka na ushindi mfululizo katika mechi zake saba za mwisho.
Social Plugin