Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ZITTO KABWE MATATANI TENA..TAKUKURU YAMUITA

Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe, ameingia matatani tena safari hii akiitwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuhusu mambo aliyoandika kwenye mitandao ya kijamii.


Taarifa iliyotolewa na Takukuru jana ilisema kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo, Brigedia Jenerali John Mbungo, amemtaka Zitto Kabwe kufika ofisini kwake akatoe ushahidi wa tuhuma alizotoa kuwa kampuni tatu za chuma kuwa zimewahonga baadhi ya viongozi wa serikali.


Takukuru katika taarifa yake hiyo ilisema wameamua kumwita Zitto baada ya kusoma kwenye mitandao ya kijamii taarifa aliyoisambaza juzi akitoa shutuma hizo.


Alifafanua kuwa taarifa hiyo ilikuwa ikielezea hisia za kuwapo kwa vitendo vya rushwa katika mradi wa uzalishaji wa chuma Liganga na Mchuchuma.


“Taarifa hiyo ambayo imewasilishwa kupitia ukurasa wa ‘Jamii Forum’ inasomeka kama imetolewa na Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Mjini,” ilisema taarifa hiyo ya Takukuru.


Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kampuni tatu za chuma kutoka China, Russia na Uturuki, zimewahonga baadhi ya watendaji wa serikali kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji na Ofisi ya Rais kwa lengo la kuchelewesha ukamilishaji wa mradi wa Mchuchuma na Liganga hadi ujenzi wa mradi wa reli ya kisasa (SGR) utakapokamilika.


Taasisi hiyo ilisema baada ya kupokea taarifa hiyo, ilifanya jitihada za kuwasiliana na Zitto kwa njia ya simu bila mafanikio.


Ilisema lengo la kumtafuta lilikuwa kujiridhisha iwapo ni kweli yeye ndiye aliyetoa taarifa hiyo na pili ni kuhitaji ushirikiano wake katika kushughulikia suala hilo.


“Tunatoa taarifa hii kupitia vyombo vya habari kumwomba Zitto Kabwe afike ofisi za Takukuru Dar es Salaam mapema iwezekanavyo ili tushirikiane katika kulishughulikia suala hili muhimu kwa mustakabali wa maendeleo ya taifa letu,” ilieleza taarifa hiyo.


Aidha, Takukuru inaendelea kuwashukuru wananchi na wazalendo wa Tanzania ambao wamekuwa mstari wa mbele kushirikiana nao katika kufichua vitendo vya rushwa na ufisadi pamoja na wanaojihusisha na vitendo hivyo bila woga.


“Hatua hii inaonyesha uzalendo wa Watanzania kuunga mkono jitihada za Rais John Magufuli katika kutokomeza kero ya rushwa nchini. Tunasisitiza wananchi kutumia njia sahihi na rasmi za kuwasilisha malalamiko dhidi ya vitendo vya rushwa ili hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa mara moja,” alisema.


Juzi, Zitto alidaiwa kuandika kuwa amepata habari za kushtusha kuwa kampuni tatu za China, Russia na Ururuki zimehonga baadhi ya watendaji wa serikali ya awamu ya tano kuchelewesha mradi wa Mchuchuma na Liganga. Lengo ni kuhakikisha nchi hizo zinapata soko la chuma chao.


Aliendelea kuandika kuwa kuhujumu mradi wa Mchuchuma na Liganga ni uhaini. Baadhi hawawezi kusahau hujuma hiyo na yoyote anayeshiriki atasakwa mpaka kaburini kwake ikibidi kuondoa kinga za watu ili iwe fundisho kwa uhujumu huu uchumi na uhai wa taifa letu.


“Msamaha wa kodi kwa bomba la mafuta kutoka Uganda ni mkubwa na hauna faida kulinganisha na mradi wa Mchuchuma na Liganga utakaotoa ajira za kudumu 35,000 kuingiza fedha za kigeni bilioni 4.6 kwa mwaka na kuifanya nchi yetu kuwa na viwanda vikubwa,” aliandika.


Zitto aliendelea kueleza katika ukurasa huo kuwa yote hayo yanafanywa chini ya uangalizi wa Rais Magufuli kiasi kwamba amelishwa matango pori dhidi ya mradi huo. Nchi yetu imegeuzwa dampo la kuagiza bidhaa za chuma kihayawani.


“Watendaji hao kutoka Wizara ya Fedha, Viwanda na Biashara na Ofisi ya Rais wamekula njama kiasi cha kuwezesha Bunge kutunga sheria kuondoa kodi zote kwa mataruma ya reli yanayoagizwa kutoka nje na kuzuia mradi wa Mchuchuma na Liganga kupata msamaha wa kodi kuwezesha mradi kuanza,” aliandika Zitto.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com