Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

3.5 BILIONI KUJENGA MAKAZI YA ASKARI DODOMA


Jumla ya nyumba Mia Moja za Makazi ya Askari zimeanza kujengwa mkoani Dodoma ikiwa ni Mpango wa serikali kukabiliana na changamoto za makazi ya Askari Polisi watakaohamia hivi karibuni baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kuanza kutekeleza agizo la kuhamishia makao makuu ya nchi mkoani hapa.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni wakati wa Ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje Ulinzi na Usalama kutembelea eneo la Medeli Mashariki ambapo Awamu ya Kwanza ya mradi huo ukihusisha nyumba 30, Ujenzi wa Shule ya Awali, Ujenzi wa Kantini, Ujenzi wa Viwanja vya Michezo tayari imeshaanza.

“Ujenzi wa nyumba hizi unakwenda sambamba na ujenzi wa nyumba kama hizi katika maeneo mbalimbali nchini ili kuhakikisha askari wanaishi sehemu safi na lengo la serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha ujenzi wa nyumba kama hizi kote nchini unafanyika kwa gharama nyepesi na tukitumia wataalamu wa ujenzi waliopo serikalini na katika Jeshi la Polisi..” alisema Masauni.

“…..mradi huu utakua na awamu tatu ambapo mwezi April mwaka jana, awamu ya kwanza ilianza na kutarajiwa kukamilika April mwaka huu huku awamu zilizobakia zikitarajiwa kukamilika mwisho wa mwaka huu na hadi kufikia mwaka kesho katikati awamu zote zitakua zimekamilika” aliongeza Masauni.

Akizungumza katika ziara hiyo Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje Ulinzi na Usalama, Mussa Zungu amewapongeza Viongozi wa wizara na Jeshi la Polisi kwa mradi huo huku akishauri miradi mingine wajenge maghorofa ili kuweza kuitumia ardhi waipatayo kwa matumizi mengine sambamba na ujenzi wa makazi ya askari.

“Nawapongeza kwa kutumia mapato yenu wenyewe ya ndani kuanzisha miradi mikubwa kama hii na sisi wajumbe wa kamati tumeridhishwa na hatua hizi za kukabiliana na makazi ya wapiganaji wetu wanaotulinda usiku na mchana na nchi yetu kuendelea kuwa na amani,” alisema Zungu.

Jumla ya gharama ya mradi huo wa nyumba Mia Moja za Makazi ya Askari Polisi ni Bilioni Mia Tatu na Laki Tano ambazo zinatokana na Mfuko wa Tuzo na Tozo ikiwemo malipo ya huduma mbalimbali zinazotolewa na askari polisi na faini zinazotozwa na askari kwenye makosa mbalimbali.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com