Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MWANAMKE AUAWA KISHA KUFUNGIWA NDANI YA BANDA LA NG'OMBE


Mkazi wa Kijiji cha Luhega, Wilaya ya Tanganyika, Milembe Manoni (22), amekutwa ameuawa kwa kuchomwa na kisu kifuani, kisha mwili wake kufungiwa ndani banda ng’ombe.


Akizungumzia tukio hilo jana, kaka wa marehemu, Nestory Malongo alisema lilitokea juzi usiku nyumbani kwa marehemu.

Alisema taarifa ya kuuawa kwa Milembe aliipata saa tatu asubuhi na wasamalia wema,

Baada ya kupata taarifa hizo, alikwenda eneo la tukio na kukuta watu wengi wakiwa wamekusanyika nje ya nyumba.

Alisema baada ya kuona mwili hiyo, waliona majeraha sehemu za kifuani ambayo inaonyesha alichowa na kisu.

Alisema polisi walifika eneo hilo, kisha kuuchukua mwili wa marehemu kwa ajili ya kwenda kuufanyia uchunguzi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi .

Mama wa marehemu, Tuma Matine alisema alipigiwa simu na mkwe wake na kusisitiza kitendo hicho ni cha kikatili mno.

Alisema katika nyumba hiyo, binti yake alikuwa akiishi na mfanyakazi mmoja ambaye alikuwa akifanya kazi ya kuchunga mifugo ya ng’ombe.

“Nasikitika baada ya tukio hili huyu mfanyakazi hajaonekana nyumbani…inawezekana wazi ndiye aliyehusika na kifo hiki,”alisema.

Mwenyekiti wa chama cha wafugaji wa mifugo wa Mkoa wa Katavi, Mussa Kabushi alisema kumekuwapo na mauaji ya mara kwa mara ya kuuawa kwa wafugaji.

Alisema mauaji hayo, yamekuwa yakisababishwa kutokana na tabia ya wafugaji kukaa kwenye maeneo ya kujitenga na kutokuwa na ulinzi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Damas Nyanda alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo na kusema jeshi hilo linaendelea na uchunguzi.
Na Walter Mguluchuma – Katavi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com