Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Job Ndugai, ametoa kauli yake baada ya Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Zuberi Kabwe kulalamika kutishiwa uhai na mtu wa usalama wa Taifa ndani ya viwanja vya Bunge siku ya jana Januari 18, mpaka kufikia hatua ya kumuandikia Spika Barua.
Spika Ndugai amesema kwamba barua hiyo haijamfikia rasmi mezani kwake ingawa kaiona mitandaoni, hivyo hawezi kuifanyia kazi mpaka pale itakapofika mezani kwake.
“Barua haijanifikia, unajua baadhi ya matatizo tunayapata siku hizi tunayakimbizia kwenye mitandao, inatakiwa niipate rasmi kama ni ya kweli tutayafanyia kazi”, amesema Spika Ndugai.
Akiendelea kuzungumzia suala hilo Spika Ndugai amesema licha ya taarifa hizo usalama wa Wabunge uko 'guaranteed”, ingawa taarifa hizo sio za kuzipuuzia.
“Usalama wa wabunge uko 'guaranteed', wabunge wako salama kabisa, kumbuka Wabunge wote kwa ujumla wetu tuko 363, na tuna watumishi pale bungeni zaidi ya 300, kwa hiyo kuna 'community' ya watu mia sita, ukisikia mtu mmoja analalamika, wawili kwenye kundi kubwa kiasi hicho, unatakiwa ulifikirie hilo jambo, sio la kudharau hata kidogo, lakini halimaanishi kwamba hapo mahali usalama haupo, pako salama sana”, amesema Spika Ndugai.
Licha ya hayo Spika Ndugai amekanusha tuhuma za kuwazima wabunge wa upinzani pale wanapotaka kuibua hoja ya msingi kuhusu muswada wa vyama vya siasa, na kusema kwamba wakati huu wadau (wananchi) ndio wanatoa maoni yao, na wao utakapofika muda wao wataruhusiwa kutoa maoni yao, hivyo wawaache wananchi wautumie muda wao.
“Hakuna wabunge wa upinzani wanaozimishwa, kwa sababu kinachoendelea sasa hivi Kamati inasikiliza wadau, Watanzania wanakuja pale kwenye Bunge wanatoa maoni yao kuhusu ule muswada, Wabunge wanapoingia mule ndani na kuanza kuleta fujo maana yake nini wakati hii sio zamu yao wao!? Zamu yao itakuja kwenye bunge mule, sasa wao wanakuja wanaanza kuleta fujo”, amesema Spika Ndugai.
Credit:Eatv
Social Plugin