Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NYAMA YA DHAHABU YAMPONZA KIUNGO WA BAYERN MUNICH FRANK RIBERY



Franck Ribery

Klabu ya soka ya Bayern Munich imepiga faini kiungo wake Franck Ribery baada ya kutuma mfululizo wa 'tweets' mbalimbali zinazoleta sintofahamu mtandaoni.

Ribery alichapisha video inayomuonesha akifurahia mnofu mkubwa wa nyama uliyopambwa na dhahabu katika mgahawa mmoja huko Dubai unayomilikiwa na mpishi maarufu raia wa Uturuki, Nusret Gokce, ambaye pia anajulikana kama "Salt Bae" kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter.

Baada ya kushambuliwa na wafuasi wake, mchezaji huyo, raia wa Ufaransa, mwenye umri wa miaka 35, aliamua kujibu ukosoaji huo kutoka kwa wafuasi wake na kuzua tafrani iliyowashtua hadi uongozi wa Bayern.

Mkurugenzi wa michezo wa klabu hiyo, Hasan Salihamidzic hakuelezea kiasi gani Ribery alikuwa ametozwa lakini alieleza vizuri kuwa faini hiyo ni "nzito".

"Alitumia maneno ambayo hatuwezi kukubaliana nayo na kwamba Franck hana haki ya kutumia kama hayo, kwakuwa yeye ni mfano wa kuigwa katika jamii na ni mchezaji mkubwa," amesema Mkurugenzi wa klabu hiyo alipoongea na waandishi wa habari Jumapili iliyopita.

"Mimi nilikuwa na mazungumzo marefu na Franck na nikamjulisha kwamba tuna nia ya kumtoza faini nzito na yeye alikubali," aliongeza.


Katika video hiyo, Ribery alionekana akisonga mikono yake kwenye mnofu huo mkubwa, ambao umeripotiwa kuwa na thamani ya Dola 340, ambazo ni sawa na shilingi laki 7 za kitanzania.

"Mafanikio yangu ni juu ya yote, shukrani kwa Mungu, mimi, na wapendwa wangu ambao waliniamini," alisema Ribery katika moja ya machapisho yake.

Salt Bae anamiliki migahawa kadhaa ya kifahari huko Marekani, Mashariki ya Kati na Uturuki, na video zake za kuchora nyama zimeangaliwa na mamilioni ya watu mtandaoni.

Amewahi kuwahudumia mastaa kadhaa, ikiwa ni pamoja na wachezaji kama Cesc Fabregas na Kevin de Bruyne. Aliwahi pia kuchapisha picha zake mwenyewe akiwa na Rais wa Venezuela, Nicolás Maduro katika mgahawa wake wa Istanbul mnamo Septemba mwaka uliopita.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com