Wabunge watano wanatarajia kufungua kesi ya kikatiba kuiomba Mahakama Kuu ya Tanzania kutoa tafsiri ya kisheria juu ya mipaka ya kinga ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na mamlaka ya Spika wa Bunge.
Wabunge hao ni Zitto Kabwe (Kigoma Mjini), Salome Makamba (Viti Maalumu), Hamidu Bobali (Mchinga), Saed Kubenea (Ubungo) na Anthony Komu (Moshi Vijijini).
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Zitto amesema wamemuagiza Wakili wao Fatma Karume kuisajili kesi hiyo chini ya hati ya dharura.
"Tutaenda Mahakamani ili kupata tafsiri ya kisheria kuhusu ni wakati gani Spika anatakiwa kumuita mwananchi yoyote kwenda kwenye kamati ya Kinga, Maadili na Madaraka ya Bunge, je atahitaji Azimio la Bunge au yeye tu binafsi na tafsiri hiyo irekodiwe.
"Kama Spika anaweza kumuita mtu mwenye kinga ya kikatiba kwa 'style' ile vipi mwananchi wa kawaida? Tumeomba tafsiri hiyo ili kulinda uhuru wa maoni, Mahakama ikisema yuko sawa sisi tutaheshimu maamuzi lakini akisema hayuko sawa nawaomba nao wakubali" Amesema Zitto na kuongeza;
"Katibu Mkuu wa mabunge ya Jumuiya ya Madola (CPA) ameniandikia kuwa tayari ameshasilisha suala langu kwa Mwenyekiti wa CPA pia amewasiliana na Spika wa Bunge la Cameroon ili ashauriane na Spika wetu kushughulikia suala la CAG bila ya kuvunja katiba"
Hivi karibuni, Spika wa Bunge, Job Ndugai, alimuagiza CAG, Profesa Mussa Assad kuripoti kwenye Kamati ya Kinga na Maadili ya Bunge, kuhojiwa kwa madai ya kulidhalilisha Bunge.
Social Plugin