Chadema imetuma mawakili wake katika Gereza la Segerea kufuatilia afya ya mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe ambaye jana alishindwa kufika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kusikiliza kesi inayomkabili, ikielezwa kuwa ni mgonjwa.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu jana alisema taarifa za kuumwa kwa Mbowe ambaye pia ni mbunge wa Hai zimewashtua kwa sababu walikuwa hawajui.
Alisema kutokana na taarifa hiyo wamelazimika kuwatuma mawakili kwenda gerezani ili kujua ni kitu gani kinachomsumbua na kujua kama amepatiwa huduma zinazostahili na kama kuna kitu kinachohitajika.
Taarifa za ugonjwa wa Mbowe zilitolewa mahakamani hapo na wakili wa Serikali mwandamizi, Patrick Mwita, wakati kesi ya ya jinai inayomkabili yeye na viongozi wengine wanane wa chama hicho mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri ilipotajwa.
Social Plugin