Unaweza kusema Spika wa Bunge, Job Ndugai ameamua kula sahani moja kimataifa na kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe.
Hiyo ni kutokana na jana Alhamisi Januari 10, 2019, Ndugai naye kuandika waraka kwenda kwa katibu mkuu wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola (CPA) kutoa ufafanuzi kuhusu barua iliyoandikwa na Zitto jana kwenda katika jumuiya hiyo.
Katika barua hiyo, ambayo Zitto amewatumia pia maspika wote wa nchi wanachama wa CPA na wanasheria wakuu, amesema sakata hilo lilianza baada ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad kusema anaamini kuwa kutotekelezwa kwa ripoti anazozitoa, ni udhaifu wa Bunge.
Wakati barua ya Zitto kwenda kwa katibu mkuu wa CPA, Akbar Khan ikieleza mzozo ulioibuka kati ya Ndugai na Profesa Assad, waraka wa Ndugai umesema Bunge hilo haliwezi kuingilia mambo ya ndani ya Tanzania.
Zitto, ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Mjini, amesema maoni hayo yamemfanya Spika Ndugai kumtaka Profesa Assad kufika mbele ya kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ili ahojiwe na kujieleza.
“Mimi binafsi nimeguswa na suala hili. Naomba mabunge ya Jumuiya ya Madola muingilie kati si tu kwa sababu agizo la Spika Ndugai linavunja Katiba bali pia ni hatari kwa mustakabali wa Jumuiya ya Madola kwa ujumla,” ameandika Zitto katika barua hiyo.
Zitto amesema kama CAG ataadhibiwa na kamati ya Bunge kwa kutoa maoni yake, basi ni wazi kwamba uhuru wa Taasisi ya Juu ya Ukaguzi (SAI) utakuwa umevunjwa, kinyume na makubaliano yaliyofikiwa na kwenye mkutano wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Madola mwaka 2013.
Na Cledo Michael, Mwananchi
Social Plugin