Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jimbo la Ukonga kimemvua uanachama diwani wa viti maalum manispaa ya Ilala, Dorcus Lukiko kwa madai ya kukihujumu chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania.
Akizungumza na vyombo vya habari leo Jumapili Januari 6, 2018 mwenyekiti wa Chadema jimbo la Ukonga, Omary Sweya amesema Lukiko amevunja kanuni na katiba ya chama kwa kutoshiriki vikao mbalimbali vya chama na kutosimamia sera zake kama katiba inavyoelekeza.
Amesema Lukiko ambaye pia mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Guluka Kwalala, amedhihirika kukihujumu chama hicho wakati wa uchaguzi mdogo katika jimbo hilo, uliofanyika Septemba 16, 2018.
"Ameonekana pia baada ya uchaguzi mdogo akimzungusha maeneo mbalimbali aliyekuwa mgombea wa CCM kwa lengo la kuwashukuru wananchi kwa ushindi alioupata bila kujali hujuma alizopata mgombea wetu na chama kwa ujumla," amesema Sweya.
Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa Lukiko amekuwa akiwadhalilisha na kuwatuhumu viongozi wa chama bila kufuata taratibu na kanuni za chama kama zinavyoelekeza.
Amesema alitumiwa barua ya kuitwa mbele ya kamati tendaji ya jimbo lakini kwa dharau alitupa barua hiyo na kutoa maneno ya kejeli kwa viongozi na chama kwa ujumla.
"Kwa niaba ya kamati tendaji ya jimbo iliyoketi kikao Januari 5, napenda kuwataarifu kwamba kuanzia sasa ninapozungumza, Dorcus Lukiko si mwanachama wa Chadema. Tunatoa tahadhari kuwa kazi zozote zitakazofanywa na yeye, Chadema isihusishwe kwa namna yoyote ile," amesema.
Social Plugin