Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI KUTOA BILIONI 5 KUKAMILISHA UJENZI WA HOSPITALI YA RUFANI SHINYANGA

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, inatarajia kutoa zaidi ya Shilingi bilioni tano kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Shinyanga, ili ianze kufanya kazi ya kutoa huduma ya matibabu kwa wananchi, na kuwaepushia gharama kubwa za kwenda kutibiwa kwenye hospitali ya Bugando, jijini Mwanza. 

Hospitali hiyo ilianza kujengwa rasmi mwaka 2014, ikiwa imeshakamilika jengo la utawala pekee kwa gharama ya Sh. bilioni 1.6.

Waziri wa wizara hiyo, Ummy Mwalimu, alisema hayo wakati alipofanya ziara ya siku moja mjini hapa kukagua ujenzi huo, Kituo cha Afya Kambarage na huduma za matibabu katika hospitali ya mkoa huo.

Alisema ukamilishwaji wa ujenzi wa hospitali hiyo ni muhimu, hivyo serikali itatoa Shilingi bilioni tano, ili kukamilisha majengo muhimu ya kutolea tiba, na ifikapo Julai Mosi, mwaka huu ianze kufanya kazi ya kutoa matibabu kwa wananchi.




"Mpaka sasa tumeshatenga Sh. bilioni 2.5 ambazo zitajenga majengo mawili ya mama na mtoto na Sh. bilioni 3.7 bado tunasubiri fedha zake ambazo zitajenga jengo la uchunguzi lenye vyumba vitatu vya upasuaji," alisema Ummy.

"Nataka niifanye hospitali hii ya rufani ya Mkoa wa Shinyanga kuwa ya kisasa kabisa, na wananchi kutokwenda kutibiwa Bugando tena, nitaweka vifaa tiba vya kisasa ikiwamo CT-Scan, pamoja na kuajiri madaktari bingwa wanane wa magonjwa mbalimbali ikiwamo ya wanawake na watoto ili kumaliza vifo vya uzazi," alisema.

Katika hatua nyingine aliwataka wananchi wa mkoa huo kujiunga na Mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii CHF iliyoboreshwa, ili kuwapunguzia gharama kubwa za matibabu na hasa pale wanapougua ghafla na kujikuta hawana pesa, hali ambayo itasaidia kupata tiba bure na kuokoa maisha yao.




Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Rashid Mfaume, akisoma taarifa ya mkoa huo, alisema kuna jumla ya zahanati 199, vituo vya afya 22, hospitali sita na ujenzi wa hospitali hiyo ya rufani ambayo imekoma kwenye jengo la utawala, pamoja na upungufu wa watumishi asilimia 52 na madaktari bingwa 21 na waliopo sita pekee.

Na Marco Maduhu - NIPASHE

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com