Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetoa wito kwa wapiga kura kwenye uchaguzi mdogo wa kata tatu utakaofanyika kesho (Jumamosi: 19.01.2019) kujitokeza kwa wingi kupiga kura ili kuwachagua viongozi wanaowataka wawaongoze kwa kipindi kilichobaki kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao.
Akisoma risala kuhusu uchaguzi huo Jijini Dar es Salaam leo (Tarehe 18.01.2019) Mwenyekiti wa Tume, Jaji (Rufaa) Semistocles Kaijage amesisitiza kwamba watakaoruhusiwa kupiga kura ni wale waliojiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Jaji Kaijage alizitaja kata zenye uchaguzi kuwa ni pamoja na Kata ya Magomeni katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni Jijini Dar es salaam, Kata ya Mwanyahina katika Halmashauri ya Wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu na Kata ya Biturana katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo Mkoani Kigoma.
“Kesho Jumamosi tarehe 19 Januari, 2019, ni siku ya Kupiga Kura katika Uchaguzi Mdogo wa Udiwani katika kata tajwa. Jumla ya Wapiga Kura 26,282 katika Vituo vya Kupigia Kura 69 watahusika na uchaguzi huu mdogo wa Udiwani,” alisema.
Jaji Kaijage amewaasa viongozi wa vyama vya siasa, wagombea, wafuasi wao na wananchi kwa ujumla wajiepushe na vitendo vinavyoweza kusababisha fujo au vurugu wakati wa uchaguzi.
“Pale panapokuwa na malalamiko yoyote ya ukiukwaji wa sheria na taratibu za uchaguzi, malalamiko hayo yawasilishwe kwenye mamlaka inayohusika kwa utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa sheria,” amesema.
Jaji Kaijage amesema kwamba upigaji kura utafanyika katika vituo vilevile vilivyotumika wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na kuongeza kwamba vituo vitafunguliwa kuanzia saa moja kamili (1:00) asubuhi na kufungwa saa kumi kamili (10:00) jioni.
“Iwapo wakati wa kufunga kituo watakuwepo wapiga kura katika mstari, ambao wamefika kabla ya saa kumi jioni na hawajapiga kura, wataruhusiwa kupiga kura. Mlinzi wa kituo cha kupigia kura, atasimama nyuma ya Mpiga kura wa mwisho aliyekuwepo kituoni kabla ya saa 10 jioni. Mtu yeyote hataruhusiwa kujiunga katika mstari wa wapiga kura baada ya muda huo,” ameelekeza Jaji Kaijage.
Licha ya kusisitiza kwamba watakaoruhusiwa kupiga kura ni wale tu ambao wamo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwenye Kata husika na wana kadi ya mpiga kura, Jaji Kaijage alisema kwamba Tume imeruhusu matumizi ya vitambulisho mbadala.
“…..Tume kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 62(a) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, imeruhusu wapiga kura ambao wamepoteza kadi zao za kupigia kura au zimeharibika au zimechakaa watumie mojawapo ya vitambulisho vifuatavyo; Pasi ya Kusafiria, Leseni ya Udereva au Kitambulisho cha Uraia kinachotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA),” amesema Jaji Kaijage.
Alifafanua kwamba mpiga kura ataruhusiwa kutumia vitambulisho hivyo, kwa sharti kwamba jina lake liwemo katika orodha ya Wapiga Kura katika kituo anachokwenda kupiga kura na lifanane kwa herufi, maneno na tarakimu na majina yaliyopo katika kitambulisho mbadala.
Jaji Kaijage alisema kwamba Tume imewaelekeza watendaji wa uchaguzi vituoni wawape kipaumbele wagonjwa, watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali, wanawake wajawazito au wenye watoto wachanga na wazee.
Pia ameelekeza kwamba mpiga Kura mwenye ulemavu wa kutoona, ataruhusiwa kwenda kituoni na mtu atakaemchagua mwenyewe kwa ajili ya kumsaidia kupiga kura.
“Wapiga kura wanatakiwa kuondoka vituoni baada ya kupiga kura na wajiepushe na mikusanyiko au mikutano katika maeneo ya vituo vya kupigia kura..,” ameagiza.
Social Plugin