CHANGAMOTO ZAAINISHWA UTEKELEZAJI SERIKALI MTANDAO


Kaimu katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Micky Kiliba akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha Serikali mtandao kilichofanyika leo jijini Dodoma
Kaimu katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Micky Kiliba walio kaa (wa nne kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa kikao kazi cha Serikali mtandao

Picha na Alex Sonna-Dodoma

Serikali imesema kuwa bado kuna changamoto zinazokabili utekelezaji wa serikali mtandao ambapo baadhi ya mifumo ya Tehama kuendelea kutowasiliana na kutobadilishana taarifa ndani ya taasisi na kati ya taasisi na taasisi.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Dk, Laurean Ndumbaro kwenye hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na kaimu katibu mkuu Micky Kiliba wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha serikali mtandao kilichofanyika hapa jijini Dodoma.

Dk, Ndumbaro amesema kuwa kuna mafanikio mengi yaliyopatikana kupitia wakala wa serikali mtandao ikiwemo kufanyika kwa uwekezaji mkubwa kwenye miundombinu ya Tehama kama vile mkongo wa Taifa, vituo vya kitaifa vya data na kutenga masafa ya intaneti ya Serikali.

Aidha amesema kuwa pamoja na mafanikio hayo lakini bado kuna changamoto ya urudufu wa mifumo ambapo kila taasisi inakuwa na juhudi za kipekee katika kusimika na kutumia mifumo na miundombinu ya Tehama ambayo ingeweza kutumiwa na taasisi zaidi ya moja.

“Baadhi ya sababu zilizochangia uwepo wa changamoto hizi ni pamoja na kutozingatia miongozo na kanuni za usimamizi wa serikali mtandao zilizopo, upungufu wa wataalamu wa Tehama wenye uwezo na ujuzi wa kutosha, misukumo kutoka kwa wafanyabiashara na wafadhili na uratibu
hafifu wa shughuli za Tehama ndani na kati ya taasisi za serikali,”amesema Dk.Ndumbaro

Hata hivyo Dk.Ndumbaro amebainisha kuwa lengo kuu la utekelezaji wa serikali mtandao ni kuboresha utoaji wa huduma kwa umma, kuimarisha utawala bora na kuongeza tija na ufanisi katika uendeshaji wa taasisi za umma kwa kuhakikisha uwepo wa mawasiliano ya haraka yenye uhakika na salama ndani na taasisi mbalimbali za serikali.

Kwa upande wake Kaimu katibu Mkuu, Micky Kiliba amewataka Watumishi wa umma kuutambulisha mfumo huo kwa serikali mtandao kwa wananchi ili kuwapunguzia gharama za kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya kufuata huduma.

Kiliba amesema kuwa wananchi wakielimishwa kuhusiana na serikali mtandao watakuwa wanapata huduma mbalimbali za kiserikali kwa kupitia simu zao za mkononi kwa kuwa lengo la kuanzishwa kwa wakala wa serikali mtandao ni kusogeza huduma karibu na wananchi.

“Hata katika masuala ya uwekezaji hakutakuwa na haja ya wawekezaji kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya kupata taarifa za uwekezaji watakuwa wanaingia kwenye mfumo wetu na kujua kila kituwanachokihitaji bila hata ya kuja huku,” amesema Kiliba.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post