Mlinda mlango mkongwe nchini Juma Kaseja, amekuwa kwenye kiwango bora siku za hivi karibuni, akiiongoza KMC kukaa katika nafasi ya 3 kwenye ligi kuu soka Tanzania bara, baada ya kutoruhusu kufungwa bao katika mechi 3 mfululizo.
Ubora wa Kaseja ulionekana alipoiongoza timu yake kushinda mabao 2-0 dhidi ya African Lyon kabla ya kushinda 1-0 dhidi ya JKT Tanzania na kumaliza mechi tatu mfululizo bila kufungwa waliposhinda 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting.
Katika mchezo wa 4 Kaseja aliruhusu mabao 2 huku timu yake ikishinda mabao 5-2 dhidi ya Coastal Union ya Tanga. Hivyo mkongwe huyo aliyewahi kuzichezea Simba na Yanga kukamilisha dakika 360 za kucheza lakini akiwa ameruhusu mabao 2 pekee.
KMC sasa ipo juu ya Simba ikiwa na alama 34 katika nafasi ya 3 na Simba wakiwa na alama 33 katika nafasi ya 4. KMC wamecheza mechi 22 huku Simba wakiwa wamecheza mechi 14.
Kaseja mwenyewe amewahi kuweka wazi kuwa bado ana mpango wa kuichezea timu ya taifa na kwa kiwango chake cha sasa huenda ikawa ni miongoni mwa machaguo ya Emmanuel Amunike.
Endapo Kaseja ataitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars, atakumbana na upinzani mkali kutoka kwa mlinda mlango namba moja wa Simba na Stars Aishi Manula ambaye naye anafanya vizuri na klabu yake.
Social Plugin