KIKOSI cha Yanga, leo kimepoteza mchezo wake wa kombe la SportPesa ikiwa ni hatua ya robo fainali kwa kukubali kufungwa mabao 3-2 dhidi ya KK Sharks ya Kenya mchezo uliochezwa Uwanja wa Taifa.
Michuano ya SportPesa Cup ambayo kwa sasa ni msimu wake wa tatu imeshirikisha timu nane ikiwa ni nne kutoka Tanzania ambazo ni Singida United, Simba, Mbao na Yanga na zile za kutoka Kenya ni pamoja na KK Sharks, Bandari, AFC Leopards na Gor Mahia ambao ni mabingwa watetezi.
Kipindi cha kwanza Yanga walikubali kupoteza kutokana na uzembe wa mabeki ambapo dakika ya 9 KK Sharks waliandika bao la kwanza kupitia kwa Abuye Duke na baada ya kuzidisha mashambulizi wakaandika bao la pili dakika ya 37 kupitia kwa Abege George.
Mpaka kipindi cha kwanza kinakamilika Yanga walikuwa nyuma kwa mabao mawili, kipindi cha pili baada ya kufanya mabadiliko kwa kumtoa Haruna Moshi na kuingia Amiss Tambwe pamoja na Abdallah Shaibu na kuingia Thaban Kamusoko, Mrisho Ngassa nafasi yake kuchukuliwa na Deus Kaseke pamoja na Paul Godfery nafasi yake kuchukuliwa na Juma Abdul kasi ya Yanga ilianza kuonekana.
Yanga walifanikiwa kurejea kwenye mchezo na kufanikiwa kufunga bao la kwanza dakika ya 87 kupitia kwa mshambuliaji wao Amiss Tambwe ambalo alifunga kutokana na uzembe wa mabeki wa KK Sharks na katika dakika za nyongeza Abuye Duke alifunga bao la tatu
Yanga hawakukata tamaa walifanikiwa kufunga bao la pili kupitia kwa Herieter Makambo katika dakika za nyongeza na kutokea fujo kwa muda ambayo mwamuzi aliimaliza na kuendelea na mpira.
Kwa matokeo hayo Yanga wanaungana na Singida United ambao nao walitolewa na Bandari kwa kufungwa bao 1-0 na wanapishana na fuko la hela za kombe hilo ambazo ni dola 30,000 pamoja na kucheza na timu ya Everton ya England.
Kesho timu mbili kutoka Tanzania zitakuwa kazini kwenye michuano hiyo ambayo ni Simba watacheza na AFC Leopards na Mbao watacheza na Gor Mahia Uwanja wa Taifa.
Via >Saleh Jembe
Via >Saleh Jembe
Social Plugin